• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
NASA kuwatia adabu wabunge wake walioshiriki kuwapiga msasa mabalozi

NASA kuwatia adabu wabunge wake walioshiriki kuwapiga msasa mabalozi

Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Bw John Mbadi akihutubia wanahabari awali. Picha/ Maktaba

Na SAMWEL OWINO

MUUNNGANO wa NASA huenda ukawaadhibu wabunge ambao walishiriki katika shughuli ya kuwapiga msasa watu walioteuliwa makatibu wa wizara na mabalozi na Rais Uhuru Kenyatta.

Muungano huo ulikuwa umepitisha kauli ya kutoshiriki katika zoezi hilo.

Wanachama wa NASA katika Kamati ya Bunge Kuhusu Teuzi walisusia shughuli ya kuwapiga msasa mawaziri tisa, ambapo pia walikuwa wametoa maagizo kama hayo kwa wabunge wanaohudumu katika kamati zingine za Bunge.

Muungano umesisitiza kuwa haumtambui Bw Kenyatta kama rais halali, hivyo kushiriki katika zoezi hilo ni sawa na kumuunga mkono.

Upigaji msasa wa makatibu na mabalozi ulifanywa na kamati mbalimbali za Bunge, ambapo baadhi ya wabunge wa upinzani walihudhuria.

Na licha ya tishio hilo, ingali kubainika aina ya adhabu ambayo wabunge hao watakabiliwa nayo.

Hata hivyo, uongozi wa Bunge katika muungano huo unatarajiwa kukutana baadaye wiki hii ili kutathmini suala hilo kwa undani.

“Ingawa maagizo kuhusu upigaji msasa wa mawaziri yalikuwa wazi, hali ni tofauti kuhusu upigaji msasa wa makatibu na mabalozi, kwani maagizo hayo hayakutolewa kikamilifu. Hata hivyo, tunaliangazia suala hilo kwa undani,” akasema Bw Junet Mohamed, ambaye ndiye Kiranja wa Wachache katika Bunge.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Wachache katika Bunge John Mbadi alisema kuwa atachukua orodha ya wale waliohudhuria shughuli hizo na kuchukua hatua kali dhidi yao.

 

Kukiuka msimamo wa chama

“Ningetaka kujua walioshiriki, sababu kuu ya kukiuka msimamo wa muungano licha ya maagizo hayo kutolewa wazi. Baadhi yao walinipigia simu wakiniuliza ikiwa wanapaswa kushiriki ambapo niliwaambia hawapaswi. Hilo linaashiria walifahamu msimamo wa chama,” akasema Bw Mbadi.

“Msimamo wetu kama ODM na NASA unabaki kwamba hatumtambui Uhuru Kenyatta kama rais, hivyo hawapaswi kuonekana kutambua uhalali wa Bw Kenyatta kama rais,” akaongeza.

Mkurugenzi wa Masuala ya Siasa katika ODM Bw Opiyo Wandayi alisema kwamba hatua ya NASA kutoshiriki katika zoezi ilikuwa wazi kwa kila mbunge.

“Wabunge ambao walikaidi agizo hilo lazima wajitokeze wazi. Ni lazima nidhamu ya vyama vya kisiasa izingatiwe,” akasema Bw Wandayi.

Baadhi ya wabunge ambao walikaidi maagizo hayo ni Caleb Amisi (Saboti), Lilian Gogo (Rongo), Patrick Makau (Mavoko), Justus Kizito (Shinyalu), Ahmed Kolosh (Wajir Magharibi), Wafula Wamunyinyi (Kanduyi), Benson Momanyi (Borabu), Charles Gimose( Hamisi) na Beatrice Adagala (Vihiga).

  • Tags

You can share this post!

Wazee sasa wamgeukia Mungu amalize njaa

Tetesi Kidero atawania ugavana Homa Bay baada ya ushindi wa...

adminleo