• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Wanasoka saba waliokosea kuondoka Barcelona wakiwemo Neymar na Bravo

Wanasoka saba waliokosea kuondoka Barcelona wakiwemo Neymar na Bravo

Na CHRIS ADUNGO

LIONEL Messi si supastaa wa kwanza wa Barcelona kuwahi kufichua azma ya kuondoka uwanjani Camp Nou kwa matumaini ya kutamba zaidi kwingineko.

Nyota huyo raia wa Argentina anatarajiwa kuagana rasmi na Barcelona mwishoni mwa msimu huu baada ya mkataba wake kutamatika.

Zaidi ya kukiri kwamba Barcelona watahitaji miujiza kurejea kuwa kikosi bora zaidi duniani, Messi, 33, ameanika ukubwa wa kiu ya kufanya kazi kwa pamoja na kocha Pep Guardiola anayehusishwa na uwezekano mkubwa wa kushawishi Messi kutua ugani Etihad kuvalia jezi za Manchester City muhula ujao.

Mbali na Man-City, Messi ambaye ni mshindi mara sita wa taji la Ballon d’Or, anahusishwa pia na PSG ambao wanawania fursa ya kushuhudia fowadi huyo akicheza pamoja na Neymar kwa mara nyingine. Neymar aliondoka Barcelona mnamo 2017 kwa kima cha Sh26 bilioni, fedha zilizomfanya kuwa sogora ghali zaidi duniani.

Hata hivyo, wapo wanasoka saba ambao waliwahi kukatiza uhusiano wao na Barcelona na visu vya makali yao vikaishia kuwa butu.

NEYMAR

PSG (AGOSTI 2017)

Ingawa Neymar aliondoka Barcelona ili kujitoa kwenye kivuli cha Messi na kuwa mwanasoka tegemeo kwingineko, nyota ya fowadi huyo raia wa Brazil haijang’aa jinsi ilivyotarajiwa kambini mwa PSG.

Kusajiliwa kwake kulichochea na matumaini kwamba angalifanya PSG kuwa miamba wa soka ya bara Ulaya kwa kipindi kirefu huku Neymar akijitia kwenye kundi moja na Messi na Cristiano Ronaldo ambao wanajivunia idadi kubwa ya mataji ya Ballon d’Or.

Hata hivyo, kubwa zaidi ambalo Neymar anajivunia kambini mwa PSG ni kusaidia waajiri wake hao kutinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2019-20 ambapo walizidiwa maarifa na wapambe wa soka ya Ujerumani, Bayern Munich.

Neymar ambaye amekuwa mwepesi wa kupata majeraha mabaya, anahusishwa na uwezekano wa kuondoka PSG na kuyoyomea Juventus ya Italia au Bayern kwa matarajio ya kutwaa taji la pili la UEFA baada ya lile la kwanza alilojizolea akichezea Barcelona mnamo 2015.

CLAUDIO BRAVO

Manchester City (AGOSTI 2016)

Katika kipindi cha misimu mitatu ndani ya jezi za Barcelona, kipa huyu raia wa Chile aliwajibishwa mara 75.

Hata hivyo, katika msimu wake wa mwisho kambini mwa Barcelona, Bravo alijipata katika ulazima wa kusugua benchi huku nafasi yake ikitwaliwa na Marce-Andre ter Stegen.

Bravo alijiunga na Man-City kwa Sh2.4 bilioni ila akakashifiwa pakubwa kutokana na masihara katika mchuano wake wa kwanza dhidi ya Manchester United.

Bravo kwa sasa anachezea Real Betis ya Uhispania kwa matarajio ya kufufua makali yake.

BOJAN

AS Roma (JULAI 2011)

Alipojiunga na Barcelona, Bojan alipigiwa upatu wa kuwa miongoni mwa wanasoka tegemeo zaidi ugani Camp Nou.

Bojan ndiye aliyevunja rekodi ya Messi ya kuwa mchezaji mchanga zaidi kuwahi kuchezea Barcelona katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) akiwa na umri wa miaka 17 na siku 19 pekee.

Hata hivyo, Bojan alijipata akisugua benchi baada ya kushindwa kuhimili ukubwa wa mawimbi ya ushindani kutoka kwa David Villa, Pedro na Messi.

Kabla ya kujiunga na Montreal Impact ya Canada inayoshiriki Major League Soccer (MLS), Bojan aliwahi pia kuvalia jezi za Milan, Ajax na Stoke City.

VICTOR VALDES

Manchester United (JANUARI 2015)

Mlinda-lango huyu alikuwa sehemu ya kikosi kilichovunia Barcelona idadi kubwa ya mataji muhimu.

Akivalia jezi za miamba hao, Valdes aliwajibishwa mara 535 na akajitwalia jumla ya mataji sita ya La Liga na matatu ya UEFA.

Mkataba wake ulipotamatika rasmi ugani Camp Nou mnamo 2014, Valdes alijiunga na Man-United alikowajibishwa mara mbili pekee kabla ya kutumwa Standard Liege ya Ubelgiji kwa mkopo.

HRISTO STOICHKOV

Parma (JULAI 1995)

Nguli huyo raia wa Bulgaria alitwaa taji la Ballon d’Or akivalia jezi za Barcelona mnamo 1994. Akifahamika kwa upekee wa kuwatoka wapinzani kirahisi na kutumia nguvu nyingi zaidi kuwakabili, Stoichkov alifunga jumla ya mabao 108 kutokana na mechi 214.

Ushawishi wake uwanjani ulisaidia Barcelona kutia kapuni mataji manne ya La Liga mfululizo na ufalme wa UEFA mnamo 1991.

Hata hivyo, alinunuliwa na Parma kwa Sh1.4 bilioni mnamo 1995 alikochezeshwa mara saba pekee katika jumla ya mechi 30.

Japo alirejea Barcelona mwaka mmoja baadaye, Stoichkov hakujivunia makali aliyokuwa nayo awali.

DECO

Chelsea (JUNI 2008)

Deco aligeuka kuwa kipenzi cha mashabiki wa Barcelona pindi aliposajiliwa kutoka FC Porto ya Ureno.

Aliambulia nafasi ya pili nyuma ya Andriy Shevchenko katika tuzo za kuwania mshindi wa taji la Ballon d’Or mnamo 2004 na akatawazwa Mchezaji Bora wa Barcelona mwishoni mwa kampeni za msimu wa 2004-05.

Mwaka mmoja baadaye, Deco alisaidia Barcelona kunyanyua ubingwa wa UEFA na akatawazwa Kiungo Bora wa Mwaka kwenye kampeni za soka ya bara Ulaya.

Hata hivyo, makali yake yalididimia pindi alipotua ugani Stamford Bridge kuchezea Chelsea waliomsajili kwa kima cha Sh1.1 bilioni. Kufurushwa kwa kocha Luiz Felipe Scolari kulimshuhudia Deco pia akitupwa nje ya kikosi cha kwanza cha Porto kwa sababu ya kushuka kwa ubora wa fomu yake.

PATRICK KLUIVERT

Newcastle United (JULAI 2004)

Mnamo 1998, Kluivert alijiunga na Barcelona katika hatua iliyomkutanisha tena na kocha Louis van Gaal aliyewahi kumtia makali kambini mwa Ajax nchini Uholanzi.

Aliibuka mfungaji bora wa Barcelona katika kipindi cha misimu mitatu kati ya sita akisakata soka ya kulipwa nchini Uhispania.

Mnamo 2004, Kluivert alipania kujaribu bahati yake kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na akasajiliwa na Newcastle United.

Hata hivyo, hakuvuma jinsi ilivyotarajiwa huku akifunga mabao sita pekee katika msimu mzima wa 2004-05.

You can share this post!

Hellen Obiri na Daniel Simiu kukosa mkondo wa mwisho wa...

Wizi wa mifugo wazidi kijijini Ngoingwa