• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
Spurs wapepeta Leeds United 3-0 na kuruka hadi nafasi ya tatu kwenye jedwali la EPL

Spurs wapepeta Leeds United 3-0 na kuruka hadi nafasi ya tatu kwenye jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

SON Heung-min alifunga bao lake la 100 akivalia jezi za Tottenham Hotspur na kusaidia kikosi hicho cha kocha Jose Mourinho kupepeta Leeds United 3-0 katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi.

Ushindi huo wa Spurs ulikuwa wao wa kwanza kusajili tangu Disemba 6, 2020. Ni matokeo ambayo yaliwapaisha hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 29, nne pekee nyuma ya viongozi wa Liverpool na Manchester United.

Hata hivyo, pointi zinazojivuniwa na Spurs zinawiana na zile ambazo Leicester City na Everton pia wamejizolea kutokana na mechi 16 zilizopita ligini.

Kwa upande wao, Leeds walisalia katika nafasi ya 11 kwa pointi 23, tatu nyuma ya West Ham United waliozamisha chombo cha Everton kwa 1-0 mnamo Januari 1, 2021 uwanjani Goodison Park.

Ingawa Spurs ndio walioibuka washindi wa mechi hiyo, Leeds ya kocha Marcelo Bielsa walicheza soka safi ya kujituma katika kipindi cha pili ila wakashindwa kukamilisha pasi za mwisho ambazo vinginevyo zingewapa mabao.

Masihara ya kipa Illan Meslier yaliwapa Spurs fursa ya kujiweka uongozini kupitia penalti baada ya Ezgjan Alioski kumchezea visivyo kiungo Steven Bergwijn. Penalti hiyo ilifumwa wavuni na nahodha Harry Kane katika dakika ya 29.

Kane alichangia bao la pili lililofungwa na Spurs kupitia kwa Son katika dakika ya 43 kabla ya Toby Alderweireld kufunga kwa kichwa na kuwapa Spurs bao lao la tatu dakika saba baadaye.

Hata hivyo, Spurs walipatwa na pigo mwishoni mwa mechi hiyo baada ya beki Matt Doherty aliyesajiliwa kutoka Wolves mwanzoni mwa msimu huu wa 2020-21 kuonyeshwa kadi ya pili ya manjano na kufurushwa uwanjani katika dakika ya 92.

You can share this post!

FUNGUKA: ‘Sina ubaya, langu ni kuhudumia wenye njaa’

Waithera: Krismasi ya 2020 ni ya kwanza kuadhimishia...