• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Waithera: Krismasi ya 2020 ni ya kwanza kuadhimishia Nairobi, natumai 2021 mambo yataimarika

Waithera: Krismasi ya 2020 ni ya kwanza kuadhimishia Nairobi, natumai 2021 mambo yataimarika

Na SAMMY WAWERU

KABLA ugonjwa wa Covid-19 kutua nchini, biashara ya uuzaji wa viatu ya Margaret Waithera jijini Nairobi ilimsaidia kuzimbua riziki na kukidhi mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

Hata hivyo, Machi 13, 2020 Kenya ilipothibitisha kuwa mwenyeji wa virusi hatari vya corona, sekta mbalimbali ikiwemo ya biashara, utalii, uchukuzi, elimu, afya, kati ya nyingine zilianza kuathirika.

Biashara ya Waithera haikusazwa. “Baadaye nililazimika kuifunga, wakati ambao nilikuwa na mgonjwa nyumbani aliyenitegemea,” anadokeza.

Anasema alichukua hatua hiyo ili kutafuta njia mbadala kujiendeleza kimaisha na pia kupata hela za kutosha kusaidia mgonjwa,baada ya kuona biahara ya viatu iliendelea kukadiria hasara.

Aidha, kulingana na Waithera, 30, kwa neema za Mwenyezi Mungu alipata nafasi ya kazi katika chama kimoja cha ushirika (Sacco), jijini Nairobi ambacho hutoa huduma za usafiri na uchukuzi.

Hata hivyo, kulingana naye ni kibarua cha muda mfupi. “Nimeshikilia mmoja wa wafanyakazi, ambaye alienda kujifungua na chini ya miezi mitatu ijayo huenda akarejea,” Waithera ambaye ni mama wa mtoto mmoja mwenye umri wa miaka 10 anaelezea, akiwa mwingi wa matumaini Sacco hiyo itampa ajira ya kudumu.

“Ninaamini bidii ninazotia kazini zitagusa mabosi wangu wanitafutie nafasi kuendelea kuhudumu,” anasema.

Shirika hilo hutoa huduma za uchukuzi na usafiri kati ya Nairobi na Eldoret.

Waithera ni mzaliwa wa Nyandarua, na anasema kwamba Krismasi ya 2020 ilikuwa ya kwanza kuadhimishia Nairobi. “Hii ndiyo Krismasi ya kwanza kusherehekea nikiwa Nairobi. Krismasi za miaka ya awali nimekuwa nikiungana na familia yangu mashambani,” anasema mwanadada huyo.

Hatua hiyo anasema ilichochewa na gharama ya juu ya usafiri iliyoshuhudiwa wakati wa pilkapilka za kuelekea nyumbani, wakazi wa mijini wakisafiri mashambani kuungana na jamaa zao msimu wa Krismasi.

“Awali kabla ya corona nauli ya kuenda nyumbani (Kinangop, Kaunti ya Nyandarua) haikuwa ikizidi Sh300. Corona ilipoingia matatu zikatakiwa kubeba asilimia 60 ya idadi jumla ya wasafiri, ilipanda hadi Sh400 na nyakati zingine 500. Msimu wa Krismasi ya 2020 haikupungua Sh700,” anafafanua.

Ni gharama anayohoji ni ya juu, akisema kiwango cha mshahara anaolipwa kisingemuwezesha kusafiri mashambani kipindi hicho.

“Nina mtoto na karo inanisubiri. Isitoshe, hupiga jeki wazazi wangu,” anasema.

Shule zinafunguliwa mnamo Jumatatu, Januari 4, Rais Uhuru Kenyatta akiagiza wazazi wahakikishe kila mtoto amerejea shuleni.

Aidha, shule zote nchini na taasisi za elimu ya juu zilifungwa mwezi wa Machi 2020 kufuatia mlipuko wa Covid-19 nchini.

Waithera anasema badala ya kujilimbikizia gharama aliamua ni heri kusherehekea Krismasi jijini Nairobi, wazazi na mwanawe akiwatumia pesa.

Mwanawe ambaye ni mvulana anaishi na wazazi wake Kinangop, Kaunti ya Nyandarua.

“Nitaenda wakati ada ya usafiri itakuwa imeshuka, kwa sasa ninashughulikia mwanangu arejee shule,” anasema.

Waithera anaendelea kueleza kwamba Sikukuu ya Krismasi 2020, Desemba 25, alikuwa kazini, kwa kuwa utoaji wa huduma za usafiri na uchukuzi uliendelea.

Huripoti kazini kabla ya saa mbili asubuhi na kutoka majira ya jioni.

“Nilichofanya siku ya Krismasi ni kutoka kazini mapema, nikajiunga na waliojitokeza kujivinjari katika Bustani ya TRM (iliyoko eneo la Roysambu, Thika Road),” Waithera akaambia Taifa Leo kwenye mahojiano ya kipekee.

Janga la corona limesababisha kuwepo kwa changamoto chungu nzima, huku wengi wakiathirika baada ya kupoteza nafasi za kazi.

“Mwaka uliopita mambo yalikuwa magumu, biashara zimeathirika kwa kiasi kikubwa. Nilikata kauli kuadhimishia Krismasi ya mwaka huu na familia yangu Nairobi,” anasema Paul Kagiri, akieleza kwamba kwa sasa anajishughulisha kutafutia wanawe karo.

“Shamrashamra za Krismasi huhusishwa na matumizi mabaya ya fedha, nitayataja kama mazishi ya pesa. Mwaka wa 2020 haukutania yeyote, watu wanapaswa kuwajibika katika matumizi ya fedha,” Kagiri anashauri.

Licha ya kupanda kwa nauli hata zaidi ya mara dufu, kuna waliosafiri mashambani kuungana na jamaa zao kuadhimisha Krismasi.

Sawa na wananchi wengine, Margaret Waithera ana matumaini mwaka wa 2021 utakuwa wenye mafanikio.

“Tumemsikia Waziri wa Afya akitangaza chanjo ya corona i njiani. Ni habari njema hasa tunapoanza mwaka,” anasema.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe ametangaza kuwa Kenya inatarajia kupokea dozi ya chanjo ya virusi vya corona kuanzia Februari 2021.

Uingereza ni kati ya mataifa ambayo yameibuka na chanjo ya Covid-19, ugonjwa ambao umekuwa janga na kero la kimataifa.

  • Tags

You can share this post!

Spurs wapepeta Leeds United 3-0 na kuruka hadi nafasi ya...

Ratiba ngumu kwa Juventus mnamo Januari 2021. Je,...