• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
MARY WANGARI: Juhudi za pamoja zinahitajika kufanikisha utekelezaji wa CBC

MARY WANGARI: Juhudi za pamoja zinahitajika kufanikisha utekelezaji wa CBC

Na MARY WANGARI

RAIS Uhuru Kenyatta hivi majuzi alizindua ripoti ya Jopokazi la Mtaala Mpya wa Elimu (CBC) katika hatua iliyoandaa jukwaa la kufanyia mageuzi muhimu sekta ya elimu nchini.

Hatua hiyo ilijiri wakati ufaao hasa ikizingatiwa kuwa CBC inasheheni manufaa mengi yatakayowezesha vijana nchini kujihami kwa ujuzi na maarifa ya kukabiliana na karne ya 21.

Iwapo mtaala huu utatekelezwa ipasavyo, ni bayana kuwa utawezesha vijana, ambao ndio viongozi wa kesho kuchangia kikamilifu kijamii, kiuchumi na kisiasa.Hata hivyo, ili kufanikisha viambajengo muhimu katika mfumo huo mpya wa elimu nchini, mikakati madhubuti inahitajika itakayoshirikisha juhudi za pamoja kutoka kwa wadau husika.

Kuna vigezo muhimu ambavyo ni sharti vishughulikiwe kwa makini ili kutimiza malengo ya CBC na hatimaye kufurahia matunda yake.Miongoni mwa vigezo hivyo ni walimu walio na jukumu muhimu katika utekelezaji wa mageuzi haya kuhusiana na sekta ya elimu.

Walimu ndio wanaokabiliwa na kibarua kigumu cha kuwezesha mtaala huo kwa uhalisia kwa kutoa mafunzo na kuwafundisha wanafunzi darasani.

Hivyo basi, ni dhahiri kuwa wanahitaji mafunzo ya kina na ya kisasa katika taasisi za elimu ikiwemo vituo vya mafunzo kwa walimu na vyuo vikuu.

Njia mojawapo ya kufanikisha hili ni kwa serikali kuwapa mikopo ya kielimu wanafunzi wanaosomea taaluma ya ualimu katika vituo vya mafunzo na vyuo vikuu.

Isitoshe, itakuwa vigumu mno kufanikisha mageuzi hayo bila kufanyia mabadiliko mfumo wote wa kutoa mafunzo kwa walimu nchini.Taasisi nyingi za kutoa mafunzo kwa walimu zingali zinatumia mifumo ya tangu miaka ya 1970 ambayo bila shaka imepitwa na wakati katika karne hii.

Ni sharti taasisi hizo zibuni mbinu mpya zinazoendana na wakati kuanzia namna ya kutoa mafunzo, muda wa kukamilisha mafunzo hayo na mahitaji mengineyo.

Aidha, ni sharti taasisi husika zihakikishe kuwepo kwa vifaa vya kisasa vya ufundishaji ikiwemo maafisa waliohitimu ili kutoa mafunzo bora kwa walimu.

Wizara ya Elimu tayari imeanzisha juhudi za kubuni sera na mikakati itakayohakikisha mageuzi yenye usawa, ubora, na yaliyo mwafaka katika sekta ya elimu.

Kigezo kingine muhimu ni nyanja ya kisiasa na kijamii inayohusisha waunda sera, wazazi na walezi ambao ni sharti wawe mstari wa mbele kufanikisha mageuzi haya.

Waundaji sheria wana jukumu la kubuni sheria muhimu kuhusu ufadhili na utekelezaji kwa kutathmini kwa makini mapendekezo ya jopokazi la CBC katika ripoti hiyo.Jamii kwa upande wake ina wajibu wa kutoa mazingira mwafaka ili kupiga jeki utekelezaji wa CBC.

Muhimu zaidi ni kuepuka kuingiza siasa duni ambazo zinaweza kuhujumu fursa hii muhimu ya kubadilisha sekta ya elimu nchini.

You can share this post!

Helikopta na magari ya kifahari viongozi wakimenyana wiki...

Tisho la baa la njaa kutokana na ukosefu wa maji Lamu