• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 4:26 PM
CHARLES WASONGA: Rais Kenyatta, Mama wa Taifa na Kagwe sasa wachanjwe

CHARLES WASONGA: Rais Kenyatta, Mama wa Taifa na Kagwe sasa wachanjwe

Na CHARLES WASONGA

IMEKUWA kawaida ya Rais Uhuru Kenyatta kwa kuwa wa kwanza kushiriki shughuli au mipango muhimu ya kitaifa kama njia ya kujenga imani ya Wakenya na kudhihirisha uongozi.

Pia amekuwa akifanya hivyo kama ishara ya kuzindua michakato hiyo, haswa inayofadhiliwa kwa fedha za umma, kwa lengo la kutoa nafasi kwa viongozi wengine na wananchi kwa ujumla kufuata nyayo zake.

Kwa mfano, mnamo Aprili 25, 2019 Rais Kenyatta alikuwa wa kwanza kujisajili kwa mpango wa Huduma Namba unaolenga kuhifadhi maelezo yote ya Wakenya katika mfumo dijitali ili wapate huduma za serikali kwa urahisi.

Mama wa Taifa Margaret Kenyatta pia alisajiliwa kisha wakafuata wengine kama vile Naibu Rais William Ruto na viongozi wa upinzani.Ama kwa hakika hatua hiyo iliondoa kabisa dhana na nadharia potovu zilizokuwa zikienezwa na baadhi ya viongozi wa kidini kwamba Huduma Namba ni nambari ya kishetani inayoelezewa katika Biblia, kitabu cha Ufunuo (Agano Jipya).

Hivi majuzi tulimwona Rais Kenyatta akiwa Mkenya wa kwanza kutia saini Mswada wa marekebisho ya Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) katika ukumbi wa KICC, Nairobi.

Baadaye aliongoza kampeni ya kuwarai Wakenya kutia saini zao katika Mswada huo ili kufanikisha mchakato huo unaofadhiliwa kwa fedha za umma; sawa na Huduma Namba.

Nimetoa mifano hii miwili kuhimili tasnifu yangu kuwa Rais Kenyatta anapaswa kupokea chanjo dhidi ya Covid-19 ili kuondoa tashwishi miongoni mwa Wakenya kuhusu usalama wa chanjo hiyo ya AstraZeneca.

Wiki jana, Wakenya waliingiwa na hofu kuhusu usalama wa chanjo hiyo iliyoendelea kupewa wahudumu wa afya, walinda usalama na walimu. Hii ni baada ya mataifa ya Denmark, Norway, Iceland, Austria kati ya mengine ya Ulaya kusitisha chanjo kwa muda pindi ilipobainika kuwa baadhi ya waliopewa walipatwa na tatizo la kuganda kwa damu.

Hakikisho la Rais Kenyatta kwa Wakenya, katika hotuba yake ya Ijumaa, kwamba chonjo hiyo ni salama halitoshi hata! Anapaswa ajitokeze hadharani ili achanjwe hadharani mbele ya kamera za wanahabari ndiposa Wakenya wawe na imani kwamba chanjo hii ya AstraZeneca haina madhara inavyodaiwa.

Ama kwa hakika, mzazi hawezi kuwatuma wanawe wakapewe chanjo ambayo yeye mwenyewe hajaipata. Kwanza, aipate kisha watoto wafuate mfano wake. Mzazi hapa ni Rais Kenyatta na watoto ni sisi Wakenya.

Rais Kagame

Hivi ndivyo, Rais Paul Kagame wa Rwanda alifanya Alhamisi wiki jana alipojitokeza hadharani kupewa chanjo dhidi ya Covid-19.Picha zilizosambazwa katika mtandao wa kijamii, Twitter, zilionyesha Bw Kagame, 63, na mkewe Jeannette wakichanjwa licha ya kwamba jumla ya watu 230,000 tayari walikwisha kupewa chanjo hiyo wakati huo.

Vile vile, mnamo Machi 1, 2021 Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo alikuwa Rais kwa kwanza barani Afrika kupewa chanjo hiyo ya AstraZeneca inayosambazwa bila malipo kwa mataifa yasiyo tajiri ulimwenguni. Mkewe Rebecca pia alipewa chanjo hii kabla za jumla ya dozi 600,000 kusambazwa kote nchini Ghana.

Kwa hivyo, japo zaidi ya Wakenya 60,000 tayari wamepewa chanjo hiyo, ninaamini kuwa Rais Kenyatta na mkewe Margaret bado wanaweza kujitokeza na kuchanjwa hadharani.

Waziri Mutahi Kagwe pia ajitokeze kushiriki shughuli hiyo yenye umuhimu kitaifa.Ikiwa baadhi ya magavana wamejitokeza na kupewa chanjo hiyo hadharani, sembuse Rais Kenyatta na Waziri Kagwe!

[email protected]

You can share this post!

Amri ya kusitisha mikutano yapoza joto la kisiasa

Walimu wote wepewe chanjo ya Covid-19 bila ubaguzi