• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Magavana Kenya wamwomboleza Rais Magufuli

Magavana Kenya wamwomboleza Rais Magufuli

WANGU KANURI NA SAMMY WAWERU

BARAZA la Magavana nchini Kenya Alhamisi limetuma risala za rambirambi kumwomboleza Rais John Magufuli wa Tanzania aliyeafariki Jumatano jioni.

Katika ujumbe wake, mwenyekiti wa baraza hilo Bw Martin Wambora, aliye pia gavana wa Embu alisema Bw Magufuli atasalia kuwa kielelezo kwa viongozi Afrika Mashariki kwani aliwahudumia wananchi wa Tanzania kwa kujitolea na bidii isiyo na kifani.

“Kwa niaba ya baraza la magavana na serikali za kaunti zote 47, ningependa kuzitoa risala zetu za rambirambi kwa wananchi wa Jamhuri ya Tanzania kufuatia kifo cha Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli. Fikira na maombi yetu inawaendea wanafamilia wake, jamaa na watu wa Tanzania ambao aliwahudumia kwa bidii na kujitolea kwingi. Tunaungana nanyi katika uombolezaji na pia katika kuyasherehekea maisha ya kiongozi huu wa kupigiwa mfano,” ikatsema taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari.

Bw Wambora aliongeza kuwa rais huyo atakumbukwa kama kiongozi mchapa kazi ambaye alitetea utawala wa kisheria nchini Tanzania.

Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wa Rais, Dkt William Ruto, kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kati ya wengineo pia wametuma risala za pole.

Huku utawala wa Dkt Magufuli ukisifiwa kutokana na jitihada zake kupambana na mafisadi, alikuwa akikosolewa na wapinzani wake kwa kile walimtaja kama dikteta.

Baada ya mkurupuko wa janga la Covid-19 nchini humo na Ukanda wa Afrika Mashariki 2020, Dkt Magufuli alipinga kuwepo kwa virusi vya corona Tanzania, akidai “tumevishinda kupitia maombi”.

Hata hivyo, Rais Magufuli Februari 2021 alisaliti amri na kukubali corona ipo Tanzania, kufuatia ongezeko la visa vya maambukizi.

Mwaka uliopita, alisimamisha kutolewa kwa takwimu za maambukizi Tanzania na pia kuzima vyombo vya habari dhidi ya kuangazia Covid-19.

Kifo chake kilitangazwa na Makamu wa Rais Samia Hassan Suluhu baada ya uvumi kugubika hali ya afya ya Rais huyo wa Tanzania kwa takriban majuma matatu alipokosa kuonekana hadharani.

Katika hotuba yake kwa taifa saa tano za usiku Jumatano, Bi Suluhu alisema kuwa Rais huyu alifariki kutokana na ugonjwa wa moyo.

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Tusipuuze athari za corona hata...

Rais Kenyatta atangaza siku 7 za kumwomboleza Magufuli,...