• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
TZ YAPATA SULUHU BAADA YA POMBE

TZ YAPATA SULUHU BAADA YA POMBE

Na MARY WANGARI

ALIYEKUWA naibu rais nchini Tanzania Bi Samia Suluhu Hassan sasa ndiye rais wa sita kuongoza taifa hilo la Afrika Mashariki baada ya kuapishwa rasmi kama rais Ijumaa.

Bi Suluhu mwenye umri wa miaka 61, alilishwa kiapo jana saa nne asubuhi katika ikulu jijini Dar-es-Salaam, kwenye hafla iliyohudhuriwa na viongozi na wajumbe wakuu, wakiwemo marais waliostaafu wa taifa hilo.

Kufuatia kiapo chake, Naibu Rais huyo aliingia katika vitabu vya kihistoria kama rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania, rais wa kwanza Tanzania ambaye ni mzaliwa wa Kisiwa cha Zanzibar na rais wa kwanza mwanamke katika bara la Afrika Mashariki kwa jumla.

Bi Suluhu ambaye vilevile aliandikisha historia kama makamu wa rais wa kwanza mwanamke Tanzania na Afrika Mashariki, alikula kiapo chake siku mbili tu baada ya kutangaza kifo cha aliyekuwa rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli.

“Mimi Samia Suluhu Hassan, naapa kwamba, nitakuwa mwaminifu, kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuitumikia kwa moyo wangu wote na kwamba nitaihifadhi, nitailinda na kuitetea katiba ya Jamhuri ya Tanzania kwa mujibu wa sheria iliyowekwa,”alisema, huku akiwa amevalia buibui jeusi na mtandio mwekundu.

Akihutubia taifa baada ya kuapishwa kwake, Bi Suluhu alisema japo alikuwa bado anaomboleza kifo cha rais, aliwahakikishia Watanzania kuwa marehemu Magufuli alikuwa amemfunza na kumwandaa vyema na kwamba alikuwa tayari kuendeleza kazi yake.

Bi Suluhu, ambaye ndiye Naibu Rais wa kwanza kuapishwa kama rais Tanzania, alivikwa cheo hicho kuambatana na Katiba ya Tanzania inayoruhusu Naibu Rais kuchukua usukani endapo rais ataaga dunia akiwa angali mamlakani.

Aidha, katiba ya Tanzania inampa mamlaka Bi Suluhu kupendekeza makamu wake baada ya kujadiliana na chama chake, Chama Tawala cha Mapinduzi (CCM).

Makamu wa rais anayependekezwa na rais mpya ni sharti athibitishwe kwa kupigiwa kura bungeni zisizopungua asilimia 50 ya kura zote.

Mama huyo wa watoto wanne, anatarajiwa kuliongoza taifa hilo kwa muda uliosalia hadi 2025, katika hatamu ya pili ya miaka mitano ambayo Rais Magufuli alikuwa amehudumu kwa miezi mitano pekee kabla ya kifo chake.

Uongozi wa Rais Suluhu unatazamiwa kuwa tofauti na utawala wa Bw Magufuli aliyepachikwa jina “bulldozer” kutokana na tabia yake ya kutekeleza sera kimabavu, ujasiri wa kwenda kinyume na sera za kimataifa hasa kuhusiana na mikakati dhidi ya Covid-19, iliyomvutia sifa tele na shutuma kali kwa usawa.

Wadadisi wameashiria kuwa, Bi Suluhu atakabiliwa na shinikizo kali kutoka kwa wandani wakuu wa marehemu Magufuli katika CCM ambao wanasimamia ujasusi na masuala muhimu ya kiserikali.

Hali hiyo huenda ikawa changamoto kwake katika juhudi za kufanya maamuzi na kuendeleza ajenda zake.

Mnamo Alhamisi, wanasiasa wa upinzani wakioongozwa na kiongozi wa Chama cha Act Wazalendo Zitto Kabwe, walitoa wito kwa Bi Suluhu kuapishwa rasmi kama rais wakisema, hatua hiyo itahakikisha kiti cha rais hakibaki tupu na kuzuia taharuki nchini humo.

You can share this post!

Kufeli sekondari hakukumzuia kuwa Rais

Naibu Gavana wa Kericho Susan Kikwai afariki kutokana na...