BIG 3 COAST LADIES TOURNAMENT: MTG United yajiondoa dimba la wanawake sababu ya mechi za ligi

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

MTG United FC imejiondoa kwenye mashindano ya siku moja ya Big 3 Coast Ladies Football Tournament yatakayofanyika mjini Malindi, Jumamosi. 

Kocha wa MTG United FC, Fathime Khamis amesema jana kuwa wamejitoa kwenye dimba hilo kutokana na kuwa watakuwa na mechi mbili za Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza ya soka ya wanawake itakazocheza jijini Nairobi Jumamosi na Jumapili.

Timu hiyo ya Kilifi itakutana na Mukuru Talents FC Jumamosi katika uwanja wa shule ya Embakasi Girls na kucheza na Limuru Talents FC uwanja wa shule ya Gichuru High siku ya Jumapili.

Mkurugenzi wa Mseto Afrika Limited, Jacob Mulanda amesema baada ya MTG United kujiondoa kwa sababu siku hiyo itakuwa na mechi yao ya ligi huko Nairobi, wameipa Changamwe Ladies nafasi ya kushiriki.

Klabu nne zitakazopigania taji hilo kwa mtindo wa kila timu kucheza na mwenzake na mshindi kupatikana kwa yule atakayepata pointi nyingi na kama pointi zitakuwa sawa kutaangaliwa mwenye magoli mengi ni Kilifi Ladies, Mombasa Olympic na Changamwe Ladies FC.

Mulanda amesema wanatarajia kuanza mashindano hayo mapema asubuhi uwanja wa Alaskan na kumalizika mapema jioni ili timu zipate kurudi zilipotoka. Huenda kampuni hiyo ikatayarisha mashindano mengine ya soka la wanawake wakati shule zitakapofungwa.

Washika dau wa soka la wanawake wanaipigia upatu Kilifi Ladies FC kushinda shindano hilo kutokana na matokeo ya mechi zao kushinda zote ilipozunguka jimbo la Pwani na kushinda zote lakini Olympic na Changamwe zitapigania kuondoka na ushindi kwenda nao Mombasa.

Habari zinazohusiana na hii