Ombi klabu za Pwani ya Afrika Mashariki zirudishe ushusiano wa kisoka

 
NA ABDULRAHMAN SHERIFF

OMBI limetolewa kwa uhusiano mzuri wa soka baina ya klabu za sehemu za mwambao wa Pwani wa Afrika Mashariki urudiwe mara tatizo la corona litakapomalizika kwani uhusiano huo ulisaidia pakubwa maendeleo ya mchezo huo.

Akizungumza na Taifa Leo jana, Mkurugenzi wa Ufundi wa Cosmos FC Aref Baghazally alisema ulipokuwako uhusiano wa kisoka baina ya klabu maarufu za miji ya Pwani ya Afrika Mashariki yakiwemo Mombasa, Dar es Salaam, Tanga na Zanzibar, mchezo huo uliimarika.

“Tulikuwa tukifurahikia kuziona timu kutoka Pwani ya Tanzania zikifika hapa kucheza na timu zetu maarufu za Liverpool (Mwenge) na Feisal na mara nyingine hata sisi tilkuwa tukifika huko Bongo timu zetu zinapokwenda kucheza mechi za kirafiki ama mashindano,” akasema Baghazally.

Timu ambazo zilikuwa na ushirikiano mkubwa kisoka ni za Mombasa za Liverpool (Mwenge) na Feisal na zile za Tanzania ambazo ni Young Africans na Sunderland (sasa Simba) za Dar, African Sports na Coastal Union za Tanga na Vikokotoni ya Zanzibar.

Baghazally ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu tatu za zamani za Ligi Kuu ya kenya, Coast Stars, Congo United na Dubai Bank FC amesema uhusiano wa klabu baina ya sehemu hizo za Pwani unastahili kuanzishwa upya kwa klabu zilizoko wakati huu.

Alitoa ombi kwa wahisani wajitokeze kuisaidia timu ya Congo Boys FC ipate udhamini wa kutosha na ipiganie nafasi ya kupanda kutoka Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza hadi Supaligi ya Taifa.

“Timu hii inaweza kufuata mfano wa Feisal na Mwenge kwani inategemea wachezaji wake wa hapa jimbo la Pwani bila ya kujali ni wa kabila gani,” akasema Baghazally.
Alikumbusha kuweko na uhusiano mzuri kati ya klabu za kanda hiyo ya Afrika Mashariki kwani ni sehemu muhimu ambazo ziliwahi kutoa wachezaji wengi waliochezea timu zao za taifa hasa kwenye mashindano ya Gossage Cup ambayo sasa yanafahamika kama Cecafa Senior Challenge Cup.
Wakati mmoja, timu ya Mwenge FC ambayo ilikuwa na wachezaji kadhaa wa timu ya taifa ya Kenya iliwahi kubeba Kombe kubwa la Baamura Cup huko jijini Dar es Salaam kwenye mashindano yaliyohusisha klabu maarufu za Sunderland, Vikokotoni, TPC ya Moshi kati ya nyengine kadhaa.

Habari zinazohusiana na hii