• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Eric Omondi anyenyekea, aahidi kuondoa mtandaoni video chafu

Eric Omondi anyenyekea, aahidi kuondoa mtandaoni video chafu

Na MARY WANGARI

MKUU wa Bodi ya Kusimamia Filamu Kenya (KFCB) Dkt Ezekiel Mutua, kupitia akaunti yake ya Twitter, mnamo Jumamosi, Machi 13, 2021, amempa chale Eric Omondi makataa ya saa 48 kuondoa video chafu katika mitandao yake ya kijamii la sivyo atakiona cha mtema kuni.

Alilalamika kuwa, licha ya msanii huyo kuomba msamaha na kikao cha kusuluhisha kesi dhidi yake nje ya korti, video hizo za ngono zingali zinasambazwa katika mitandao yake.

Mkurugenzi huyo wa KFCB alimwamrisha Omondi kuziondoa video hizo mara moja kwenye mitandao yake ya kijamii kufikia Jumatatu, Machi 15, 2021.

“Tulipokea ombi la msamaha na kikao cha kutatua kesi dhidi yake nje ya mahakama kutoka kwa Eric Omondi, lakini yaonekana video hizo za kuaibisha zingali zinasambazwa katika mitandao yake ya kijamii,”

“Video hizo chafu ni SHARTI ziondolewe kufikia saa mbili asubuhi mnamo Jumatatu, Machi 15, 2021, la sivyo…,”aliandika Dkt Mutua.

Akizungumza Alhamisi baada ya Omondi kuachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000, Dkt Mutua alitangaza kuwa ameteua Kamati ya Maridhiano itakayokutana na timu ya KFCB na maafisa wa DCI Jumatatu, Machi 15, 2021.

Kamati hiyo itaongozwa na mcheshi maarufu Churchill Ndambuki, mtangazaji wa redio na mcheshi Felix Odiwuor pamoja na wasanii wengine tajika.

Hii ni baada ya msanii huyo kumwomba radhi Dkt Mutua kwa kurekodi filamu zinazokiuka maadili ya kijamii na kuachiliwa kwa dhamana pamoja na waigizaji wake 15 wanawake waliotozwa dhamana ya Sh50,000 kila mmoja.

Omondi alitangaza mitandaoni kukatiza filamu yake inayofahamika kama WifeMaterial2, akiahidi kuanzisha awamu mpya ya filamu hiyo itakayokuwa na matini bora zaidi inayozingatia maadili ya kijamii.

“Nimekuwa na mawasiliano marefu kwa njia ya simu na rafiki yangu mzuri Daktari Ezekiel Mutua na amesisitiza kuwa si lazima WifeMaterial iwe chafu ili iuze. Ninakubaliana naye kabisa na nimemtumia ombi binafsi la kumwomba msamaha,”

“Lengo limekuwa daima kuburudisha na wala si kuchukiza na ningependa kumwomba radhi yeyote aliyekerwa,” alisema.

Mnamo Alhamisi, maafisa wa DCI walimkamata mcheshi huyo pamoja na waigizaji wake kwa kukiuka Sheria kuhusu Filamu na Michezo ya Kuigiza Kipengele 222 cha Katiba ya Kenya.

You can share this post!

Ombi klabu za Pwani ya Afrika Mashariki zirudishe ushusiano...

Man-United kumtia mnadani kipa David de Gea mwishoni mwa...