• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
Mamia ya wasichana wafanyia KCSE hospitali baada ya kujifungua

Mamia ya wasichana wafanyia KCSE hospitali baada ya kujifungua

Na WAANDISHI WETU

MAMIA ya watahiniwa wa kike wanafanyia mtihani wao wa Kidato cha Nne (KCSE) hospitalini kote nchini baada ya kujifungua kutokana na mimba walizopata wakati wa likizo ndefu mwaka jana kufuatia janga la virusi vya corona.

Katika eneo la Meru, Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti Milton Nzioka alisema wasichana saba wanafanyia mtihani hospitalini na wawili kati yao wako katika Hospitali ya Muthara, Tigania Mashariki.

“Wengi wa watahiniwa wa walio hospitalini wanangojea kujifungua,” akasema Bw Nzioka.Katika Kaunti ya Nyeri, watahiniwa wawili wanafanyia mtihani wao katika Hospitali ya Othaya Level Five.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Kaunti, Lyford Kibaara, mmoja wa wasichana hao amekaribia kujifungua huku mwingine akiwa na matatizo ya kiafya yaliyotokea baada ya kujifungua.

Wawili hao ni miongoni mwa watahiniwa 18,500 wanaofanya mtihani wa KCSE kwenye vituo 246 katika Kaunti ya Nyeri.Katika Kaunti ya Isiolo, wasichana zaidi ya 10 waliopachikwa mimba wakati wa likizo ndefu mwaka jana, wanafanya mtihani wa KCSE.

Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti ya Isiolo Hussein Koriyow aliambia Taifa Leo kuwa watahiniwa wote waliojifungua wanaendelea kufanya mtihani huo wa Kidato cha Nne.

“Mmoja wa watahiniwa kutoka shule moja iliyoko mjini Isiolo, alijifungua wiki mbili zilizopita. Watahiniwa wote walio na ujauzito na ambao tayari wamejifungua wanaendelea na mtihani wao,” akasema Dkt Koriyow.

Katika Kaunti ya Tharaka Nithi, mmoja wa watahiniwa alifanyia mtihani kwenye chumba cha kujifungulia katika Hospitali ya Rufaa ya Chuka.Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti Bridget Wambua jana alisema kuwa wanafunzi wote, wakiwemo wasichana wanaotarajia kujifungua hivi karibuni watafanya mtihani wa KCSE.

Jumla ya watahiniwa 10,981; wasichana 5,764 na wavulana 5,217 wanafanya mtihani wa KCSE katika kaunti hiyo.Katika Kaunti ya Migori, watahiniwa wanne walijifungua Alhamisi, siku moja kabla ya mtihani wa KCSE kung’oa nanga Ijumaa.

Watahiniwa wawili wanatoka katika eneobunge la Suna Mashariki huku wengine wawili wakitoka eneobunge la Kuria Mashariki.Mtihani wa KCSE ulianza siku mbili baada ya kukamilika kwa Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) Jumatano.

Ripoti ya GITONGA MARETE, REGINAH KINOGU, WAWERU WAIRIMU na ALEX NJERU

You can share this post!

TANZIA: Mama Sarah Obama afariki

Jambazi sugu Maragua aponea kuuawa na polisi baada ya...