Obado afufua mashambulizi dhidi ya Raila

Na JUSTUS OCHIENG

GAVANA wa Kaunti ya Migori, Okoth Obado, amefufua mashambulizi yake dhidi ya kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, akiapa kuanzisha chama kipya cha jamii za eneo la Nyanza na kukashifu vikali Mpango wa Maridhiano (BBI).

Bw Obado aliyezungumza katika sherehe ya kufungua nyumba ya Mkurugenzi wa Usimamizi wa serikali yake, Bw Dominic Akugo katika wadi ya Uriri ya Kati mnamo Jumapili, alisema kwamba anafurahia kwamba kampeni za BBI zilizovumishwa sana zimesitishwa.

Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta wamekuwa wakipigia debe mageuzi ya katiba kupitia BBI.

Mnamo Jumapili, Bw Obado alipuuza mchakato huo, akisisitiza kwamba hautabadilisha maisha ya Wakenya.

“Tunakabiliwa na matatizo mengi katika nchi hii na tuko kati kati ya janga. Tunaumizwa na gharama ya juu ya bei za bidhaa za kimsingi na hali ya maisha imekuwa ngumu,” alisema.

“Kwa hivyo, madai kwamba BBI itaimarisha maisha yetu ni uongo mkubwa. Maisha hayawezi kuwa nafuu kutokana na BBI. Tunafurahia kwamba Mungu amesimamisha reggae,” Bw Obado alisema katika kanda ya video ya dakika 18 ambayo Taifa Leo ilipata.

Gavana huyo anayehudumu kwa kipindi cha pili alitaja jinsi mabunge ya kaunti na viongozi walivyotishwa na kuhongwa ili wapitishe mswada wa kubadilisha Katiba wa 2020.

“Tulitishwa kweli kwamba iwapo mabunge ya kaunti yasingepitisha mswada huo baadhi ya watu wangekamatwa. Baadhi walitishwa kwamba wangeshtakiwa na kwa hivyo madiwani wakaamua kuupitisha,” alisema.

Bw Obado anayekabiliwa na mashtaka kadhaa kortini alifichua jinsi viongozi walikuwa hatarini iwapo wangeuliza maswali kuhusu mchakato huo.

“Sasa Mungu ametusaidia kuthibitisha kwamba ulikuwa mpango mbaya na ukiletwa hapa kupigiwa kura, ushughulikieni ipaswavyo,” alisema gavana huyo akimaanisha kura ya maamuzi iliyopendekezwa ifiwapo basi wakazi waangushe mswada huo.

Akilenga vinara wa mpango huo, gavana huyo alisema: “Kwa kaka na dada zetu wanaoshikilia nyadhifa za juu za mamlaka na nguvu, watu wanapozungumza, msiwalazimishe, msiwatishe, msiwahonge.”

“Ni makosa kwa wale wanaotekeleza haki yao ya kutoa maoni kutishwa. Hiyo si demokrasia,” Obado aliongeza huku akirejelea alivyonusurika chama cha ODM kiliposhinikiza aondolewe ofisini.

Pia, alifichua mipango ya kuunda chama kipya cha kisiasa katika eneo hilo ambalo ni ng’ome ya chama cha ODM.

Bw Obado alidokeza kwamba atatumia chama cha Peoples’ Democratic Party (PDP) kinachoongozwa na Bw Omingo Magara ambacho alitumia kushinda uchaguzi mkuu wa 2013.

“Ikiwa watu hao walikuwa wakisema BBI itaunganisha watu, na sisi tunasema kwamba PDP itatuunganisha na kuwezesha watu wetu,” alisema.

Alisisitiza kuwa kunafaa kuwepo demokrasia katika ngazi zote.

Alisema muungano wa One Kenya Alliance wa viongozi wa vyama vya kisiasa; Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC), Gideon Moi (Kanu) na Moses Wetang’ula (Ford Kenya), hauwakilishi jamii zote za Kenya na ulimuacha nje Bw Odinga na kwa hivyo “ kuna haja yetu kuunda chama ambacho kitawakilisha maslahi yetu.”

Habari zinazohusiana na hii

Wapuuza Uhuru

Raila amezea mate OKA