• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Liverpool kucheza dhidi ya Real Madrid leo usiku

Liverpool kucheza dhidi ya Real Madrid leo usiku

Na MASHIRIKA

KIVUMBI kinatarajiwa leo usiku miamba wa zamani Real Madrid na Liverpool watakapokabana koo kwenye mkondo wa kwanza wa robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), uwanjani Valdebebas mjini Madrid.

Liverpool, almaarufu The Reds, watalenga kulipiza kisasi masaibu yaliyowapata katika fainali za mwaka 2018, walipobamizwa 3-1 na wenyeji wao wa leo Jumanne.

Hususan, kumbukumbu za beki Sergio Ramos akimuangusha fowadi wao Mohamed Salah, aliyeumia vibaya bega na kuishia kuaga mchuano huo.

Kwa upande wao, Real wanatarajiwa kutumia uwanja wa nyumbani kujizolea alama zote tatu dhidi ya wapinzani wao kutoka Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Uga wa Valdebebas unatumika kwa sasa kufuatia shughuli za ukarabati zinazoendelea kwenye uwanja wao wa kawaida wa Santiago Bernabeu.

Wenyeji, wanaofahamika kama Los Blancos, wataingia uwanjani wakijivunia matokeo mazuri katika mechi za karibuni, ikiwemo ushindi wa 2-0 dhidi ya Eibar katika mechi ya La Liga mwishoni mwa wiki.

Ili kufuzu kwa hatua hii ya robo-fainali, vijana hao wa kocha Zinedine Zidane walibandua Atlanta BC ya Italia katika hatua ya 16-bora.

Hata hivyo, kocha Zidane atakosa huduma za nyota wake kadhaa wanaouguza majeraha.

Nahodha Ramos aliumia majuzi akichezea timu ya taifa ya Uhispania katika mechi ya kimataifa. Inasemekana huenda akarejea baadaye mwezi huu.

Kutokuwepo kwake kutapunguza uhondo uliotarajiwa hii leo kati yake na Salah.

Pia kuna uwezekano kiungo Eden Hazard hataingia ugani Valdebebas kwani amekuwa akisumbuliwa na jeraha la misuli.

Ingawa hivyo, huenda akawa kwenye benchi baada ya kuanza kuonyesha mabadiliko makubwa mazoezini.

Beki stadi wa kulia Dani Carvajal pia amekuwa akisumbuliwa na jeraha la mguu tangu aumie Februari wakicheza na Valencia ligini, na bado hayuko tayari kurejea uwanjani.

Katika mechi nyingine kali ya UEFA leo usiku, vinara wa EPL Manchester City watakuwa nyumbani Etihad kuvaana na Borussia Dortmund.

Vijana wa Pep Guardiola walitinga robo-fainali baada ya kubandua Borussia Monchengladbach katika hatua ya 16-bora, huku wapinzani wao wakiwazima Sevilla kwenye raundi hiyo.

Kocha Guardiola amekuwa akifutilia mbali madai ya wengi kwamba kikosi chake kipo katika nafasi nzuri ya kutwaa mataji kadhaa msimu huu.

Licha ya hayo, kwa makali wanayoshambulia wapinzani, Man-City wanapigiwa upatu kuwa na kibarua rahisi leo usiku.

City watashuka dimbani wakijivunia ushindi muhimu wa 2-0 ugenini dhidi ya Leicester City, ulioimarisha mwanya wao wa alama 14 kileleni.

Mabingwa hao wa zamani wanaongoza ligi kwa alama 74 mbele ya Manchester United (60), Leicester City (56) na Chelsea (51) wanaofunga mduara wa nne-bora wa kufuzu kwa UEFA msimu ujao.

You can share this post!

AFC: Wasiwasi kambini kuhusu kocha Aussems

Jay-Z akasirisha kwa jezi ya msikiti Lamu