• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 4:48 PM
Ramadhan: Supkem yaomba Rais asaidie Waislamu kwa chakula na fedha

Ramadhan: Supkem yaomba Rais asaidie Waislamu kwa chakula na fedha

GEORGE SAYAGIE na AFP

VIONGOZI wa Kiislamu wamemrai Rais Uhuru Kenyatta kuwasaidia Waislamu kwa chakula na fedha nchini, wakati wanaadhimisha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kaimu mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Kenya (SUPKEM), Bw Hassan Ole Naado, alisema kuwa mwezi huo huwa wakati muhimu kwa Waislamu wengi kumkaribia Mungu, familia zao na jamii kwa jumla.

Hata hivyo, alisema kuwa uwepo wa janga la corona nchini umevuruga shughuli na mipango yao mingi.

Akizungumza Jumapili, alipowahutubia wananahabari mjini Narok, alisema Waislamu wanatarajiwa kuanza mfungo wa Ramadhan leo au kesho jioni, wakati mwezi utakapoonekana.

Katika nchi za Misri na Lebanon, viongozi wa kidini walitangaza Jumapili kwamba mwezi wa Ramadhan utaanza leo.

Nchini Saudi Arabia, ambako ndiko kitovu cha dini hiyo, viongozi katika miji mitakatifu ya Mecca na Medina walisema wangekutana jana ili kujadili wakati mfungo huo utakapoanza rasmi.

Hili ni kwa kuwa mwezi haukuonekana vizuri Jumapili.

Bw Naado alisema kuwa wakazi wengi katika ukanda wa Kaskazini Mashariki ambao ni Waislamu wanakabiliwa na uhaba wa chakula, hivyo wanahitaji msaada wa serikali kwa dharura.

Alikuwa akielekea katika Kaunti ya Transmara kufungua msikiti wa 36 katika kaunti hiyo.

“Ninaiomba serikali kutoa msaada wa chakula kwa zaidi ya Wakenya milioni moja ambao wanakabiliwa na uhaba wa chakula katika kaunti zilizo katika maeneo kame. Ninamrai Rais Kenyatta kuongoza juhudi za kuwashinikiza wadau na mashirika mbalimbali kuwasaidia wakazi hao kwa fedha na chakula wakati huu muhimu katika dini hii,” akasema.

Bw Naado alieleza sikitiko lake kwamba idadi ya Wakenya wanaokabiliwa na uhaba wa chakula katika kaunti zilizo katika maeneo kame wameongezeka kutoka 700,000 hadi milioni moja mwaka huu.

Kaunti hizo ni Tana River, Wajir, Garissa, Mandela na Isiolo. Vile vile, aliwaomba Waislamu wenye uwezo kifedha kuwasaidia wale wanaohitaji misaada katika jamii.

Alisema wakazi wengi wanaoishi mijini, hasa kwenye mitaa ya mabanda pia wanakumbwa na uhaba wa chakula.

“Kama Waislamu, tunapaswa kujali maslahi ya ndugu zetu. Wale ambao wana uwezo wanapaswa kujitokeza na kuwasaidia wenzao katika maeneo wanakoishi,” akasema.

Wito huo unajiri huku serikali ikiwa imefunga shughuli za kiuchumi katika kaunti za Nairobi, Machakos, Nakuru, Kajiado na Kiambu ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

You can share this post!

Zakat Kenya kuwafaa Waislamu Ramadhan

Sonko aondoka hospitalini