• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 5:13 PM
Zakat Kenya kuwafaa Waislamu Ramadhan

Zakat Kenya kuwafaa Waislamu Ramadhan

Na CECIL ODONGO

HUKU Waislamu wakitarajiwa kuanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan kesho au Jumatano, shirika moja lisilo la kiserikali linalenga kulisha familia 6,000 katika Kaunti ya Nairobi na pia kuendeleza mpango kama huo kote nchini.

Ili kutimiza malengo hayo, shirika la Zakat Kenya linalenga kupata Sh24 milioni kutoka kwa wafadhili na watu ambao wana moyo wa kutoa msaada ili kuzifikia familia zisizojiweza wakati wa Ramadhan.

Iwapo mwezi utaonekana leo usiku basi Waislamu wataanza kufunga kesho ila ukionekana kesho basi mfungo wa Ramadhan utaanza Jumatano.

Mwenyekiti wa Zakat Kenya Ali Khalid alisema kuwa kwa sasa Wakenya wanapitia hali ngumu ya kimaisha kutokana na athari ya janga la corona na ni vyema wasiojiweza wasaidiwe kujikimu maishani.

Hata hivyo, si mara ya kwanza shirika hilo linatoa msaada kwa kuwa limekuwa likifanya hivyo kwa muda wa miaka mitano iliyopita na Bw Khalid anatoa wito kwa wahisani na wafadhili wengi wajitokeze ili wafikie familia nyingi zaidi.

Kwa mujibu wa Bw Khalid, kila familia itapewa msaada wa vyakula na bidhaa muhimu kwa kima cha Sh4,000 kuwawezesha kufuturu wakati wa Ramadhan.

“Kwa kweli hali ilivyo mara nyingi shughuli hii hufanyika misikitini na tangu ujio wa corona misikiti imefungwa na haijakuwa rahisi kuwafikia kwa kusambaza msaada huu wakati wa futari.

“Tunalenga kuhakikisha hakuna familia zinazoumia wakati wa Ramadhan kwa kukosa chakula ndiposa tunatoa wito kwa mashirika na watu wanaojiweza waje watusaidie kuzifikia eneo la Nairobi na maeneo mengine ya Kenya,” akasema Bw Khalid.

Hapo jana, malori yaliyojaa vyakula yalianza safari ya kuusambaza msaada huo katika mitaa ya Kangemi, Dandora Phase 1-5, Kamkunji, Starehe, Embakasi na Mathare. Usambazaji huo unaongozwa na makundi yanayotambulika katika mitaa hiyo.

Katibu Mkuu wa Zakat Kenya Sheikh Abdul Shakur Mohamed ambaye anasimamia kitengo cha usambazaji wa msaada huo, naye alisema kuwa shughuli hiyo itaendeshwa kwa uwazi na familia zilizotambuliwa zitapokea mgao wao.

“Shughuli hii inaendeshwa kwa uwazi na tunayaomba mashirika tunayoshirikiana nayo na mengine yaungane nasi kuwafikia watu wanaohitaji msaada. Kuna watu wengi ambao corona imesambaratisha maisha yao na hawana ajira na hii ni kati ya njia muafaka ya kuwafikia,” akasema Mohamed.

You can share this post!

Waliotia ‘mchele’ kwa pombe ya mteja wakamatwa

Ramadhan: Supkem yaomba Rais asaidie Waislamu kwa chakula...