• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Sonko aondoka hospitalini

Sonko aondoka hospitalini

RICHARD MUNGUTI na WINNIE ATIENO

ALIYEKUWA gavana wa kaunti ya Nairobi ameondoka Nairobi Hospital alipokuwa amelazwa kutibiwa baada ya kuugua akiwa mikononi mwa polisi.

Mawakili Dkt John Khaminwa , Assa Nyakundi na Wilfred Nyamu walimweleza hakimu mkuu Bw Lawrence Mugambi kwamba Bw Sonko aliondoka hospitali Alhamisi.

“Bw Sonko aliondoka hospitali Alhamisi kisha akaagizwa apumzike kwa siku 14,”Dkt Khaminwa alimweleza Bw Mugambi.

Hivyo basi, hakimu alielezwa Bw Sonko hangeweza kufika kortini kama alivyoamriwa na hakimu mwandamizi Bw Peter Ooko wiki iliyopita.

Bw Mugambi aliamuru ripoti ya kubaini utimamu wa akili ya Bw Sonko ifunguliwe na kusomwa mbele ya Bw Ooko aliyeamuru apimwe na madaktari katika hospitali kuu ya Kenyatta (KNH).

Awali malumbano makali yalizuka kati ya mawakili wa Bw Sonko na viongozi wa mashtaka kuhusu siku ile kesi inayomkabili ya ufisadi wa Sh14milioni dhidi yake na washukiwa wengine wawili itakapotajwa.

Mawakili wa gavana huyo walitaka kesi itajwe Machi 25,2021 nao viongozi wa mashtaka walitaka itajwe Machi 15,2021.

“Najua kesi dhidi ya Bw Sonko hazitaendelea. Bw Sonko ni mgonjwa. Anakabiliwa na changamoto za akili (ubongo). Hawezi keti kwa muda mrefu. Anatarajiwa kusafiri hadi Afrika kusini kufanyiwa upasuaji wa nyonga za miguu yake,” Dkt Khaminwa alisema.

Matamshi hayo yalichemsha ari na hasira za viongozi wa mashtaka waliosimama na kusisitiza sharti kesi dhidi ya Bw Sonko itajwe wiki ijayo.

Mawakili wa Sonko na viongozi wa mashtaka walifarakana mbele ya Bw Mugambi na kurushiana cheche za maneno.

“Kwa vile hamwezi kubaliana siku ya kutajwa kwa kesi dhidi ya Bw Sonko itabidi niitengee siku ya kutajwa mimi mwenyewe,”Bw Mugambi alisema.

Aliamuru kesi hiyo ya ulaghai wa Sh14milioni dhidi ya Bw Sonko itajwe mnamo Machi 22, 2021.

Bw Sonko ameshtakiwa pamoja na washukiwa wengine wawili na wako nje kwa dhamana.

  • Tags

You can share this post!

Ramadhan: Supkem yaomba Rais asaidie Waislamu kwa chakula...

Omar alitumia ‘juju’ kuzubaisha mpenziwe, korti...