Man-City wapiga Palace 2-0 na kunusia ubingwa wa EPL

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City waliwapiga Crystal Palace 2-0 uwanjani Selhurst Park na kujiweka katika nafasi ya kutwaa taji la EPL kwa mara ya tatu chini ya misimu minne iwapo Man-United watapoteza dhidi ya Liverpool mnamo Mei 2, 2021 ugani Old Trafford.

Mabao ya Man-City dhidi ya Palace yalipachikwa wavuni kupitia Sergio Aguero na Ferran Torres katika dakika za 57 na 59 mtawalia. Matokeo hayo yalisaza Palace ya kocha Roy Hodgson katika nafasi ya 13 kwa alama 38.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City wanafukuzia pia taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya kuhifadhi ufalme wa Carabao Cup muhula huu wa 2020-21.

Huku Palace wakijiandaa kuvaana na Sheffield United mnamo Mei 8, 2021 ugani Bramall Lane, Man-City watarudiana na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa kwenye nusu-fainali ya UEFA mnamo Jumanne ijayo.

Watashuka uwanjani Etihad, Uingereza wakijivunia ushindi wa 2-1 katika mkondo wa kwanza ugenini. Watapepetana na Chelsea ligini baada ya kibarua hicho dhidi ya PSG.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO