• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:19 PM
Real wakomoa Osasuna na kuwakaribia Atletico kileleni mwa jedwali la La Liga

Real wakomoa Osasuna na kuwakaribia Atletico kileleni mwa jedwali la La Liga

Na MASHIRIKA

REAL Madrid waliwapepeta Osasuna 2-0 na kuendeleza presha kwa Atletico Madrid ambao ni viongozi wa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Jumamosi usiku.

Mabao ya Real yalipachikwa wavuni kupitia Eder Militao na Casemiro kunako dakika za 76 na 80 mtawalia. Goli la Casemiro lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na fowadi matata raia wa Ufaransa, Karim Benzema.

Real ambao ni mabingwa watetezi wa La Liga walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kusajili ushindi baada ya Atletico Madrid kuwapiga Elche 1-0 awali na kuendeleza ubabe wao kwenye kampeni za La Liga muhula huu.

Atletico kwa sasa wanadhibiti kilele cha jedwali la La Liga kwa alama 76, mbili zaidi kuliko Real. Barcelona wanashikilia nafasi ya tatu kwa pointi 71, moja pekee mbele ya nambari nne Sevilla.

Eden Hazard aliyepangwa katika kikosi cha kwanza cha Real kwa mara ya kwanza tangu Januari 2021, alipoteza nafasi za wazi za kufunga huku fataki zake zikidhibitiwa na kipa wa Osasuna, Sergio Herrera.

Real ya kocha Zinedine Zidane sasa inajiandaa kupepetana na Chelsea katika mkondo wa pili wa nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Mei 5, 2021 ugani Stamford Bridge. Chelsea wataingia katika mechi hiyo wakijivunia bao la ugenini baaada ya kusajili sare ya 1-1 katika mchuano wa mkondo wa kwanza mnamo Aprili 27, 2021. Real watakuwa wakipania kutinga fainali ya UEFA kwa mara ya tano chini ya kipindi cha miaka minane.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Neymar awabeba PSG dhidi ya Lens na kuendeleza presha kwa...

Man-City wapiga Palace 2-0 na kunusia ubingwa wa EPL