• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
JAMVI: Wazee wa Pwani wanakosa sauti ya kunguruma kisiasa

JAMVI: Wazee wa Pwani wanakosa sauti ya kunguruma kisiasa

Na WAANDISHI WETU

KATIKA taifa ambalo wazee wa kijamii hujihusisha sana na siasa katika jamii nyingi, hali ni tofauti kwa wazee wa jamii za Pwani.

Wazee wa jamii kama vile za maeneo ya Kati, Bonde la Ufa, Magharibi, Nyanza na Kaskazini Mashariki huonekana mara kwa mara hasa wakati chaguzi kuu zinapokaribia wakijaribu kushawishi mkondo ambao jamii zao zinafaa kuchukua kwa siasa za kitaifa na vile vile, siasa za maeneo yao.

Imekuwa kawaida wazee wa jamii mbalimbali kugonga vichwa vya habari wakati wanasiasa wanapopanga mikakati ya kuwa wasemaji watakaowakilisha jamii zao katika siasa za kitaifa.

Katika jamii nyingine kama vile Kaskazini Mashariki, wazee hujihusisha pia kutoa mwelekeo kuhusu uongozi wa mashinani kama vile ugavana na ubunge.

Lakini katika ukanda wa Pwani, kimya cha wazee kimeibua kishindo kikuu hasa wakati huu ambapo wanasiasa wamewakanganya raia kuhusu mwelekeo wa kisiasa ambao utafaa kuchukuliwa kuelekea kwa Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Wanasiasa wangali wamegawanyika kuhusu iwapo watastahili kuunda muungano mmoja wa kupigania maslahi ya Wapwani kwani wengine wao tayari wameamua kufuata njia zao wakiungana na vigogo ambao si wa asili ya Pwani walio katika vyama tofauti.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Jumapili umebainisha kuwa, ukosefu wa umoja baina ya jamii asili za Pwani ni chanzo kikuu kinachotatiza uwezo wa wazee kutoa kauli moja ya kisiasa.

Kulingana na Katibu wa baraza la wazee katika Kaunti ya Tana River, Bw Kesi Wario, utengano wa Wamijikenda ndio chanzo halisi cha wazee kukosa kunguruma kuhusu siasa za Pwani.

Akizungumza na Taifa Jumapili mjini Garsen, Bw Wario ambaye pia ni mfalme wa jamii ya Wanyoiyaya alisema jamii za Pwani zimetofautiana na hata kudharauliana kwa misingi ya viwango vya elimu na utajiri kuliko hekima.

“Pwani hii kuna wale wanaojiona wamesoma sana na hawawezi kushauriwa na wazee ambao labda hawakuwahi kukanyaga shule ama pengine kisomo chao kiko chini. Dharau kama hizi haziwezi kuinua sauti ya Pwani,” akasema.

Jamii za Wamijikenda hujumuisha makabila ya Wachonyi, Wakambe, Waduruma, Wakauma, Waribe, Warabai, Wajibana, Wagiriama na Wadigo.

Hata hivyo, eneo hilo lina wenyeji wa makabila mengine mengi ambayo si ya asili ya Wamijikenda waliofanikiwa kujitosa katika siasa na kujizolea umaarufu mkubwa.

Mzee huyo aliongezea kuwa wakati mwingine baadhi ya wazee wanapohitajika kutoa mwongozo kisiasa, huwa wanageuka kuwa vibaraka wa wanasiasa badala ya kupigania masilahi ya umma.

“Kama tunataka kuwa wazee wa kusikika kimataifa, lazima tuweke tamaa za nafsi zetu pembeni na tujadili mwelekeo wetu kwa uwazi,” akasema.

Alitilia shaka nia ya baadhi ya wanasiasa kuunda muungano au chama cha Wapwani, akisema kuwa hakuna aliye na nia ya kufanikisha wazo hilo.

Alifananisha wazo hilo na sherehe ambapo kuna watakaotumika kama maji ya kunawa mikono na wale wa kusubiri kitoweo kipakuliwe, ambapo wananchi ndio watakuwa maji ya kunawa huku viongozi wakijongea kula minofu.

Kauli sawa na hii ilitolewa na Baraza la Wazee wa Lamu, ambao walisema wametengwa katika maamuzi ya kisiasa yanayohusu Pwani na Kenya kwa jumla.

Zaidi ya hayo, Naibu Mwenyekiti wa baraza hilo, Bw Mohamed Mbwana alisema wanasiasa, hasa wale chipukizi wamekuwa wakijitenga na mawaidha ya wazee hata wanaposhauriwa.

Bw Mbwana alisema kuwa wazee wa Lamu pia wanastahili kushirikishwa kikamilifu katika siasa za Pwani na kitaifa badala ya kubaguliwa na kuonekana kuwa watu wasiofaa.

“Utatoaje kauli kisiasa wakati hujashirikishwa? Viongozi wametutenga. Na ndiyo sababu tukaamua kukaa mabarazani tukiwatazama tu kwa macho. Watakapoafikia kutushirikisha kwenye vikao vyao hapo ndipo tutakubali kutoa mwelekeo wetu kisiasa,” akasema Bw Mbwana.

Wanachama wengine wa baraza hilo walisema mila na desturi zao haziwaruhusu kushiriki makongamano ya kisiasa ambayo huonekana kuwa ni upotovu na ulaghai kwao.

“Siasa za sasa zimekuwa za watu wanaotetea matumbo yao, kudhulumu wanyonge na kadhalika. Hatutaki kujihusisha katika maovu. Tunahisi kuchangia siasa ni sawa na kuwasaidia wanyanyasaji, mabepari na makatili kuendeleza dhuluma zao,” akasema katibu wa baraza hilo, Bw Mohamed Athman.

Hata hivyo, imebainika kuwa wazee wa Kaya wamekuwa wakihusishwa katika mazungumzo yanayojaribu kuunda muungano wa kisiasa Pwani.

Mshirikishi wa muungano wa wazee wa Kaya, Bw Tsuma Nzai alisema tayari wameunda kikundi cha wazee wa Kaya ambacho kitaongoza mchakato wa siasa za Pwani. Mwenyekiti wa kundi hilo ni Mzee Stanley Mbeo kutoka Kaya Ribe.

Bw Nzai alilaumu viongozi na wanasiasa katika eneo la Pwani kwa kutokuwa na umoja utakaohakikisha kuwa eneo hilo linakuwa na msimamo imara kisiasa kama ilivyo katika sehemu zinginze nchini ambao wanaendelea.

Kulingana na Bw Nzai, wazee wa Kaya walipendekeza kuwa Gavana wa Kilifi Amason Kingi ama mwenzake wa Kwale Salim Mvurya awe kinara wa chama au muungano utakaoundwa lakini wazo hilo likapingwa na wanasiasa wengine.

“Ikiwa sisi tunapigania kuwa na kinara wa Pwani ambaye atakuwa wa kutoka jamii ya Mijikenda ilhali Gavana Kingi akiongea kuna viongozi na wanasiasa wetu wanampinga na kumpura mawe, ni dhahiri kuwa wao ndio wenye matatizo na wanarudisha safari yetu nyuma kila kukicha,” akasema.

Kaunti nyingine za Pwani ni Mombasa, Taita Taveta, Tana River na Lamu.

Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, tayari alitangaza atapigania tikiti ya kuwania urais kupitia Chama cha ODM baada ya kupata umaarufu mkubwa kitaifa katika kipindi chote cha miaka kumi alipokuwa gavana.

Baadhi ya viongozi waliojitenga na uundaji wa muungano wa Pwani walidai wanashuku kuna njama fiche ambayo hawajaelezwa wazi.

Ripoti za Kalume Kazungu, Stephen Oduor na Maureen Ongala

You can share this post!

2022: Kuna dalili Uhuru atasema ‘Raila Tosha’

Cherotich na Kipng’etich watifulia wenzao kivumbi mbio za...