• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
Museveni ataka nchi zote za Afrika zitumie Kiswahili

Museveni ataka nchi zote za Afrika zitumie Kiswahili

Na MASHIRIKA

RAIS wa Uganda Yoweri Museveni ameyataka mataifa ya Bara Afrika yatumie lugha ya Kiswahili kudhihirisha umoja wao badala ya kuendelea kusifia na kuchangamkia lugha za kigeni.

Kiongozi huyo ambaye ameongoza Uganda kwa miaka 35 ameyataka mataifa ya Afrika yaungane pamoja na kuyapa kipaumbele maslahi ya raia wao badala ya kila mara kutegemea nchi za Wazungu kwa kila jambo.

“Wazungu wanapotaka waungane, wao hujiuliza lugha ambayo wanafaa waitumie. Je, watumie Kitaliano, Kihispania, Kiingereza au Kijerumani. Hata hivyo, barani Afrika tunaweza kutumia Kiswahili ambacho hakibagui na ni lugha ambayo haimilikiwi na mtu yeyote,” akasema Rais Museveni.

Kiongozi huyo alikuwa akizungumza katika Ikulu ya Entebe wakati wa mkutano wa kuadhimisha siku ya utangamano barani Afrika.

“Afrika tayari wameungana na hatufai kugawanyika kamwe. Ni rahisi sana kwa Waafrika kuungana kuliko wazungu ila hatujakuwa tukizingatia hilio. Tukiendelea kugawanyika basi hatutatimiza maazimio yetu,” akaongeza Museveni.

Katika miaka ya hivi karibuni, Uganda imechukua hatua za kimakusudi wa ajili ya kukuza na kuendeleza lugha Kiswahili.

Kwa mfano mnamo Oktoba, 2019 Serikali ya nchini hiyo iliidhinisha kuundwa kwa baraza la kitaifa la Kiswahili ambalo mojawapo ya wajibu wake ulikuwa kuweka mikakati ya kupandishwa hadhi ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya pili Uganda.

Waziri wa Jinsia, Ajira na Maendeleo ya Kijamii Peace Mutuzo aliwaambia wanahabari kwamba Kiswahili pia ni lugha inayotambuliwa na katiba ya nchi hiyo.

‘Katika siku za nyuma Kiswahili kilikuwa kikitumiwa na majeshi, wezi, waliokuwa wakikitumia vibaya na kufanya vurugu kwa watu na (watu) hawakukipenda Kiswahili sana. Lakini leo, tumekuwa watu wamoja katika Afrika Mashariki na tungependa kuendeleza Kiswahili’.

Bw Mutuzo alieleza kuwa uundwaji wa baraza hilo ulikuwa umepata idhini ya asasi mbalimbali za serikali na “itaanza kazi mara moja.”

“Hii ni hatua muhimu katika taifa letu kwa sababu lugha ya Kiswahili ina uwezo wa ‘kukuza jumuiya yetu na utamaduni kwani mambo mengi yanayozungumza kwa kiswahili ni mambo yanayojulikana na lugha nyingine za hapa Uganda’.

Waziri huyo alielezea imani Uganda itafanikiwa katika ndoto yake ya kuieneza na kuikuza Kiswahili, lugha ambayo tayari linafundisha katika taasisi za elimu nchini humo.’

Tuna walimu wengi ambao wamefunzwa Kiswahili na wana vyeti lakini hawajapata kazi,na tutazungumza na wizara ya elimu kuwapatia kazi waweze kufundisha Kiswahili shuleni na kwenye redio na televisheni’, akasema Waziri Mutuzo.

Baraza hilo pia lilitwikwa wajibu wa kutunga sera, mwongozo wa kisheria na kitaasisi na kuweka viwango vya kuhimizwa ipasavyo kando na kuendeleza lugha ya Kiswahili katika nyanja zote.

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Ripoti ya Kriegler itekelezwe kusaidia...

DOUGLAS MUTUA: ‘Mashujaa’ wanaoibia umma wafungwe jela