David Alaba achukua nafasi ya Sergio Ramos Real Madrid

Na MASHIRIKA

BEKI David Alaba amesema kwamba hana azma ya kuwa kizibo kikamilifu cha aliyekuwa difenda na nahodha wa Real Madrid, Sergio Ramos uwanjani Santiago Bernabeu.

Alaba ambaye ni raia wa Austria, aliingia katika sajili rasmi ya Real mnamo Mei 2021 baada ya mkataba wake kambini mwa Bayern Munich ya Ujerumani kukamilika rasmi.

Sogora huyo mwenye umri wa miaka 29 sasa amepokezwa jezi nambari nne mgongoni iliyokuwa ikivaliwa na Ramos kambini mwa Real.

Ramos aliyehudumu kambini mwa Real kwa kipindi cha miaka 16, alijiunga na Paris Saint-Germain (PSG) bila ada yoyote. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 35 alipokezwa mkataba wa miaka miwili kambini mwa PSG ambao sasa wanatiwa makali na kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino.

“Ramos alikuwa hapa kwa muda mrefu na alivalia jezi nambari nne mgongoni. Nitajituma ila huenda nisiwe kizibo chake kamili,” akasema Alaba.

Ramos ambaye anajivunia rekodi ya kuchezea Uhispania idadi kubwa zaidi ya mechi, alishindia Real mataji matano ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) akiwa Real.

Kwa upande wake, Alaba aliyetia saini mkataba wa miaka mitano kambini mwa Real, alishindia Bayern mataji 10 ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), sita ya ya German Cup na mawili ya UEFA.

Alaba atakuwa chini ya mkufunzi Carlo Ancelotti aliyerejea kambini mwa Real mnamo Juni 2021 kujaza pengo la Zinedine Zidane baada ya kuagana rasmi na Everton ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO