• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:58 PM
TAHARIRI: Uteuzi na mbinu mbovu tatizo letu

TAHARIRI: Uteuzi na mbinu mbovu tatizo letu

KITENGO CHA UHARIRI

KWA mara nyingine udhaifu wa Kenya katika maandalizi, uteuzi na mbinu za benchi la ufundi ulijidhihirisha jana pale Kenya ilipogaragazwa katika mbio ilizoshiriki.

Katika mchujo wa mbio za mita 800 uliofanyika asubuhi, ni Mkenya mmoja tu, Mary Moraa, aliyefuzu kwa hatua ya nusu fainali, ilhali taifa hili liliwakilishwa na wakimbiaji watatu katika kivumbi hicho.

Saa chache baadaye, Kenya iliondoka mikono mitupu katika mbio za mita 10,000 baada ya wakimbiaji wake kuaibishwa vibaya zaidi, yamkini vibaya zaidi katika historia ya michezo hiyo, pale washiriki wake walipomaliza katika nafasi ya saba na tisa.

Yaani wanariadha wa Kenya hawangejikakamua hata kushinda nishani ya shaba tu. Ilikuwa aibu kubwa.

Katika mbio za mita 800, ilidhihirika mapema kuwa Kenya haingeenda mbali baada ya kuteuliwa kwa baadhi ya wanariadha ambao walionekana ‘kuchoka’ hasa wanapotathminiwa kutokana na mashindano ya miaka ya majuzi hasa Riadha za Dunia za Qatar.

Swali hapa ni je, kwani chipukizi wa kukimbilia taifa hili wameisha? Je, hamna vijana wanaozaliwa tena katika kitovu cha wanariadha shupavu ulimwenguni, la Bonde la Ufa na kwingineko?

Katika mbio za mita 10,000 ilibainika kuwa mbinu mbovu bado ndizo tatizo letu kuu. Ukosefu wa mbinu kali za kutimka mbio za mafasa marefu umekuwa ukituponza kwa miaka mingi kiasi kwamba kwa zaidi ya miongo mitatu Kenya haijawahi kushinda dhahabu katika masafa hayo.

Wakenya Rodgers Kwemoi na Rhonex Kipruto walianza kuongoza mapema katika mbio za mita 10,000; mbinu ambayo ni hatari sana maadamu humchosha mshindani mapema kiasi cha kukosa mkurupuko muhimu wa dakika ya mwisho.

Mbio hizi aghalabu humhitaji mkimbiaji kuwafukuza wanaoongoza kabla ya kuchapuka katika mikondo michache ya mwisho.

Mtindo uliotumiwa na Wakenya hao jana huhitaji wakimbiaji maarufu pekee ambao hawachoki haraka ama wale ambao wanapofungua mwanya hawawezi kushikika kamwe.

Wakimbiaji maarufu kama Vivian Cheruiyot, Hellen Obiri, Almaz Ayana na Mo Farah ndio huweza kudhibiti mwendo bila kuchoka.

Hata hivyo, si rahisi kuwaona wakiongoza mbio wanazokimbia katika hatua ya mwanzo mwanzo kama Wakenya walivyofanya Ijumaa.

You can share this post!

Brazil kuvaana na Mexico katika nusu-fainali za Olimpiki...

Jamaica yazoa medali zote tatu za Olimpiki katika mbio za...