• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 7:55 PM
Jamaica yazoa medali zote tatu za Olimpiki katika mbio za mita 100 wanawake

Jamaica yazoa medali zote tatu za Olimpiki katika mbio za mita 100 wanawake

Na MASHIRIKA

MWANARIADHA Elaine Thompson-Herah aliweka historia ya kuwa mwanamke wa pili mwenye kasi zaidi duniani baada ya kumpiku mwenzake wa Jamaica, Shelly-Ann Fraser-Pryce na kuhifadhi dhahabu ya 100m wanawake jijini Tokyo, Japan.

Thompson-Herah, 29, alisajili muda wa sekunde 10.61 na kusaza sekunde 0.12 pekee kuvunja rekodi ya dunia iliyowekwa na Florence Griffith-Joyner wa Amerika miaka 33 iliyopita.

Shericka Jackson alihakikisha kwamba Jamaica wanazoa nishani zote tatu kwenye mbio hizo baada ya kuambulia nafasi ya tatu kwa sekunde 10.76, 0.02 pekee nyuma ya Fraser-Pryce.

Mshindi wa mbio za mita 100 kwa wanawake Elaine Thompson-Herah (kati) akiwa na Shelly-Ann Fraser-Pryce (kushoto) aliyemaliza wa pili na Shericka Jackson (kulia) aliyejihakikishia nafasi ya tatu Julai 31, 2021. Picha/ AFP

Daryll Neita wa Uingereza aliyepigiwa upatu wa kutatiza watimkaji hao kutoka Jamaica, alitupwa katika nafasi ya nane kwa muda wa sekunde 11.12.

Hata hivyo, Mwingereza mwenzake, Dina Asher-Smith, alishindwa kufuzu kwa fainali na akajiondoa pia kwenye 200m baada ya kuanza kutatizwa upya na jeraha la paja alilolipata mwanzoni mwa Julai 2021.

Fraser-Pryce aliyesajili muda wa kasi zaidi katika safari ya kufuzu kwa fainali, alijipata akiwa na presha tele baada ya kuanza vibaya kivumbi cha mwisho mnamo Julai 31.

Muda uliosajiliwa na Thompson-Herah baada ya kumpiku Fraser-Pryce katika hatua ya mita 30 za mwisho, ulimwezesha kufikia rekodi ya Griffith-Joyner   anayejivunia muda wa pili wa kasi zaidi duniani.

Muda huo wa Thompson-Herah ulimwezesha pia kuweka rekodi mpya ya Olimpiki katika mbio za 100m wanawake.

Thompson-Herah ambaye amekuwa akiuguza jeraha la mshipa wa mguu kwa takriban miaka mitano iliyopita, aliambulia nafasi ya tatu wakati wa mchujo wa Olimpiki uliondaliwa na Jamaica kwa ajili ya Olimpiki mwaka huu.

Jeraha hilo lilimkosesha Riadha za Dunia za Doha 2019 alizopania kutumia kama jukwaa la kujizolea nishani ya kwanza ya dhahabu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

TAHARIRI: Uteuzi na mbinu mbovu tatizo letu

Kenya yasajili visa vipya 1,259 vya Covid-19 kufikisha...