• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wakazi wahofia vita vya jamii za wafugaji

Wakazi wahofia vita vya jamii za wafugaji

Na FLORAH KOECH

WAKAZI katika maeneo yanayokabiliwa na visa vya wizi wa mifugo katika Kaunti ya Baringo wameelezea hofu kwamba hatua ya kuwafurusha wachungaji haramu katika eneo jirani la Laikipia itachochea mapigano baina ya jamii za eneo hilo.

Hii ni baada ya mamia ya wachungaji kuhamia maeneo yenye malisho mengi wakiandamana na mifugo.

Wiki mbili zilizopita, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i aliwapa makataa ya siku saba mamia ya wachungaji mifugo kutoka Isiolo, Samburu na Baringo, ambao wamevamia mashamba ya kibinafsi katika Kaunti ya Laikipia, kuhama au kufurushwa kimabavu.

Alionya kwamba ikiwa hawatatii amri kuhusu makataa hayo, ambayo muda wake tayari umeisha, serikali itaanzisha operesheni kali ya kuwafurusha.

Wakazi wa Laikipia walikuwa wameelezea wasiwasi wao kuwa walisha mifugo hao wamewapokonya mashamba yao na ndicho kiini cha ukosefu wa usalama ambao umesababisha watu kupoteza maisha na mali.

Hatua hiyo, hata hivyo, imezua taharuki miongoni mwa wakazi katika Kaunti ya Baringo huku wakidai kuwa wachungaji hao wamevamia Baringo Kusini kwa wingi na huenda wakasababisha mapigano baina ya jamii kutokana na kung’ang’ania raslimali chache zilizopo za maji na malisho.

You can share this post!

Leicester wapata beki wa kuziba pengo la Fofana...

Ni Tusker dhidi ya Arta Solar 7 anayochezea Alex Song...