• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:03 AM
Ni Tusker dhidi ya Arta Solar 7 anayochezea Alex Song kwenye Klabu Bingwa Afrika

Ni Tusker dhidi ya Arta Solar 7 anayochezea Alex Song kwenye Klabu Bingwa Afrika

Na GEOFFREY ANENE

TUSKER FC itarejea kwenye Klabu Bingwa Afrika baada ya misimu minne nje na mechi dhidi ya Arta Solar 7 ya kuingia raundi ya kwanza ya kufuzu ya msimu 2021-2022.

Katika droo iliyofanywa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) hapo Agosti 13, vijana hao wa kocha Robert Matano watalimana na timu hiyo kutoka Djibouti inayoajiri mchezaji wa zamani wa Arsenal na Barcelona raia wa Cameroon Alex Song, mnamo Septemba 10-11 na Septemba 17-18.

Mshindi ataingia raundi ya pili ya kufuzu itakayoandaliwa Oktoba 15-16 na Oktoba 22-23. Kisha, mshindi wa raundi hiyo ya pili ataingia mechi za makundi ambayo washiriki wanaanza kupokea tuzo. Mechi za makundi ni kati ya Februari 11 na Aprili 2. Zitafuatiwa na robo-fainali kati ya Aprili 15 na Aprili 21, nusu-fainali kati ya Mei 6 na Mei 14 halafu fainali itasakatwa Mei 29.

Ikiwa Tusker itabandua Arta Solar 7, itakutana na miamba wa Misri, Zamalek katika raundi ya pili.

Tusker ilipata tiketi ya kushiriki mashindano hayo ya haiba baada ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kuamua kuwasilisha jina la timu iliyokuwa imekalia juu ya jedwali la Ligi Kuu kufikia mwisho wa mwezi uliopita wa Julai.

Vijana wa Matano wangali kileleni mwa ligi hiyo ambayo imekuwa ikishuhudia ushindani mkali kati ya wanamvinyo hao na wanabenki wa KCB. Hata hivyo, Tusker walipata nafasi ya kupumua katika vita vya kutawazwa bingwa wa taifa walipocharaza Kakamega Homeboyz 2-0 Julai 13 nao KCB wakaduwazwa na Vihiga United 2-1 siku hiyo. Tusker sasa wanaongoza kwa alama 61, tatu mbele ya KCB ikisalia michuano miwili kipenga cha mwisho cha msimu 2020-2021 kipulizwe.

Katika dimba la Afrika la klabu, Tusker haikuwa na lake katika kampeni yake ya mwisho mwaka 2017. Ilibanduliwa na wanavisiwa wa AS Port-Louis 2000 kutoka Mauritius kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kukabwa 1-1 jijini Nairobi na kupoteza 2-1 ugenini.

Kabla ya hapo, Tusker iliaga makala ya 2013 katika raundi ya pili ilipopoteza nyumbani 2-1 na ugenini 2-0 mikononi mwa miamba wa Misri, Al Ahly. Wanamvinyo hao walikuwa wameaibisha St Michel United kutoka Ushelisheli 7-1 katika hatua ya kuingia raundi ya kwanza. Pia, Tusker walisalimu amri mapema katika Klabu Bingwa Afrika 2012 baada ya kulimwa na APR kutoka Rwanda 1-0 wakitafuta tiketi ya raundi ya kwanza.

You can share this post!

Wakazi wahofia vita vya jamii za wafugaji

ODM yashutumiwa kwa kupendekeza kung’olewa mamlakani...