• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 9:55 AM
Afisa ajipata taabani kwa kukejeli jaji

Afisa ajipata taabani kwa kukejeli jaji

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA wa polisi aliyechunguza kesi ya sakata ya sukari ya Sh79milioni dhidi ya wakurugenzi watatu wa kampuni ya United Millers Limited (UML) jana alijipata taabani kwa kumkejeli na kumdunisha Jaji wa Mahakama kuu ya Kisumu aliyesikiza na kuamua kesi hiyo. kuhusu hakuwa na makini.

Sajenti James Ochola alishindwa kueleza sababu ya kudai “Jaji alikuwa na haraka ya kusikiza na kuamua kesi iliyowasilishwa na UML dhidi ya kampuni ya B N Kotecha & Sons Ltd.”UML iliwasilisha kesi ikidai ilipwe zaidi ya Sh124milioni na B N Kotecha iliyoshindwa kuiuzia sukari ilhali ilikuwa imelipwa.

Akihojiwa na wakili M M Gitonga anayewakilisha Sunil Narshi Shah , Kamal Punja , Magnesh Verma , meneja wa masuala ya uuzaji Henry Kavita na UML, Sajini Ochola alishindwa kabisa kueleza sababu ya kumdunisha Jaji aliyesikiza kesi hiyo  kwa kudai “alikuwa na pupa na kutoa uamuzi kabla ya kupokea ushahidi wote.”

Bw Gitonga alimkabidhi Sajini Ochola maamuzi matatu yaliyotolewa na majaji tofauti katika mahakama kuu ya Kisumu miongoni mwao Jaji Fred Ochieng kisha akaulizwa kati ya watatu hao “nani alitoa uamuzi bila kuzingatia ushahidi na kwa pupa.”

Afisa huyo wa polisi aliyechunguza  kesi ya kula njama kulaghai kampuni ya  B N Kotecha Sh79milioni aliomba msamaha kwa makosa ya kudunisha jaji aliyesikiza kesi hiyo na kutoa uamuzi zaidi ya Sh124milioni zilipwe.

Washtakiwa Sunil Narshi Shah , Kamal Punja , Magnesh Verma , meneja wa masuala ya uuzaji Henry Kavita ..PICHA/RICHARD MUNGUTI

Kampuni ya B N Kotecha & Sons Limited ilikubali kuilipa UML zaidi ya Sh124milioni kwa kushindwa kuiuzia sukari.UML ilikuwa imesikizana na B N Kotecha iiuzie sukari magunia 42,412 kwa bei ya Sh124,106,600.

UML ilikuwa imepokea maombi kutoka kwa wafanya biashara katika eneo la Mlima Kenya iwapelekee sukari.Lakini B N Kotecha ilishindwa kuuzia UML sukari  hiyo.Kutokana na hayo mahakama kuu iliamuru B N Kotecha iilipe UML pesa ilizokuwa imepokea.

Mkurugenzi wa B N Kotecha & Sons Ltd Bw Hemal Kishor Kotecha alikiri mbele ya hakimu mkuu Bi Roseline Onganyo kwamba alilipa UML Sh124m kufuatia agizo hilo la mahakama kuu.

Makampuni hayo yalikubaliana kusuluhisha kesi hiyo nje ya mahakama.Akitoa ushahidi , Sajini Ochola,anayehudumu katika afisi ya uchunguzi wa jinai ya Ugunja kaunti ya Siaya alikanusha madai kwamba aliwasingizia wakurugenzi hao wanne walikula njama za kufuja kampuni ya  B N Kotecha Sh79milioni.

Sajini Ochola alikanusha aliamua kuwashtaki wanne hao kwa hila.Akijibu maswali kutoka kwa kiongozi wa mashtaka  Bi Everlyne Onunga , Sajini Ochola alisema  “hana kinyongo wala husuda na washtakiwa.”

Sajini Ochola alisema uamuzi wa kuwashtaki wanne hao ulitolewa na afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma.Sunil ,Punja , Vermaq , Kavita na UML wamekanusha mashtaka saba ya kula njama za kulaghai, kughushi stakabadhi za kuagiza bidhaa (LPO) kutoka kwa wafanya biashara miji ya Kerugoya , Karatina , Nyeri na Nkubu.

Kesi itaendelea Oktoba 27,2021 mahakama itakapoombwa iwaachilie washtakiwa kwa vile upande wa mashtaka umeshindwa kuthibisha kesi dhidi ya washtakiwa.

  • Tags

You can share this post!

Kaunti zatakiwa kuanzisha mpango tamba wa utoaji chanjo

Wawili washtakiwa kujifanya wanahabari