• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:55 AM
Kalonzo akosa njia, Azimio wamtarajia

Kalonzo akosa njia, Azimio wamtarajia

COLLINS OMULO Na JUSTUS OCHIENG

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka anajiandaa kurejea katika muungano wa Azimio, wiki moja tu baada ya kutangaza kujiondoa, Taifa Leo imefahamu.

Duru ndani ya chama chake cha Wiper zinaeleza kuwa Bw Musyoka hana budi kutokana na shinikizo kali ambazo amewekewa na wagombeaji viti kwa tiketi ya Wiper, ambao wamemwambia wazi wazi kuwa wataendelea kumpigia debe mwaniaji urais wa Azimio, Raila Odinga.

Wawaniaji hao wapatao 500 waliokutana Machakos, Jumatatu, walisema tangazo la Bw Musyoka wiki jana la kujiondoa Azimio na kuwa atawania urais kivyake kwa tiketi ya Wiper lilikuwa lake binafsi.

Tangazo la Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, Wafula Chebukati jana Jumatatu kuwa watafuata sheria ya vyama kuidhinisha wagombeaji pia linamaanisha itakuwa vigumu kwa Bw Musyoka kuwa debeni Agosti 9.

Bw Chebukati alidokeza kuwa ni sharti walio katika miungano wafuate maafikiano waliotia sahihi walipoungana.

“Tutafuata sheria kuhusu uchaguzi. Azimio walituletea kanuni zao na tukawapa cheti cha kuthibitisha ziko sawa. Hivyo tunatarajia wanachama kuziheshimu,” akasema Bw Chebukati.

Kulingana na mkataba wa vyama washirika katika Azimio, vyama tanzu haviwezi kujiondoa miezi sita kabla ya uchaguzi na sita baadaye. Hii itamfunga Bw Musyoka katika Azimio.

Dokezi zinaeleza kuwa kwa hofu ya kujipata kwenye baridi kampeni zikianza, Bw Musyoka atatangaza kurudi Azimio wakati wowote wiki hii.

Wandani wake walisema Jumatatu Bw Musyoka karibuni atafanya mkutano wa wakuu wa muungano huo ili kutatua tofauti zilizochangia atangaze kuwa atawanua urais kivyake.

“Tunataka kuwa sehemu ya Kenya mpya. Hii ndiyo maana tunasema kuwa bado kuna nafasi kwa kiongozi wetu kufanya mazungumzo na Azimio kwani chama chetu kinaweza kuchangia katika ufanisi wake,” katibu mratibu wa Wiper, Robert Mbui alisema Jumatatu.

Bw Mbui ambaye pia ni mbunge wa Kathiani, alisema kuwa suala hilo ni la Wiper kama chama wala sio la Bw Musyoka: “Tunataka kujua kile ambacho Wiper kama chama kitapata kwa sababu masilahi yetu kama chama ni makuu kuliko ya mtu mmoja.”

Alifafanua kuwa Bw Musyoka alitangaza kujiondoa katika Azimio sababu hakukuwa na nafasi ya kufanya mazungumzo.

Duru katika mkutano huo ziliambia Taifa Leo kwamba idadi kubwa ya wawaniaji viti wa tiketi ya Wiper wanamtaka Bw Musyoka kurejea Azimio.

Mnamo Jumatatu wiki jana, kiongozi huyo wa Wiper alitangaza kujiondoa kutoka Azimio na kuwa atawania urais kivyake baada ya mgombea urais wa muungano huo Raila Odinga kumteua kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua kuwa mgombea mwenza wake katika kinyang’anyiro cha urais Agosti 9.

Tangu atangaze kujiondoa, Bw Musyoka amekuwa akihimizwa na viongozi wa Azimio arejee katika muungano huo.

  • Tags

You can share this post!

Aliyeiba kipakatalishi kanisani atupwa jela miaka mitatu...

PSG watumia mabilioni ya pesa kushawishi Mbappe kuwaruka...

T L