• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Aliyemuua mkewe kwa kumpakulia wali bila nyama afungwa miaka 15

Aliyemuua mkewe kwa kumpakulia wali bila nyama afungwa miaka 15

NA MWANGI MUIRURI

MWANAMUME mwenye umri wa miaka 56 kutoka Kaunti ya Embu aliyemuua mkewe akilalamika kwamba alimwandalia chakula bila nyama sasa atakaa jela kwa miaka 15.

Crispin Nyaga kutoka kijiji cha Kambaru alikuwa ameshtakiwa kwa kumuua Bi Catherine Mbuya aliyekuwa mkewe, mnamo Desemba 25, 2022.

Jaji Lucy Nuguna alisoma hukumu hiyo kwa njia ya mtandao mnamo Julai 27, 2023 kwa msingi kwamba licha ya kuwa mlevi chakari, mshukiwa aliweka wazi nia ya kupanga mauaji hayo.

Nyaga alikuwa ameieleza mahakama kwamba siku hiyo ilikuwa muhimu sana kwa kuwa ilikuwa Krismasi.

“Nilikuwa nimemwachia Sh2,000 ambazo zilikuwa sehemu ya pato langu la Sh3,000 ambazo nilipata sokoni Kiritiri baada ya kuuza muguka,” akasema.

Aliporejea nyumbani akiwa mlevi, Nyaga alidai chakula lakini akashangaa kwamba licha ya kumwachia mkewe pesa za kutosha, wali alioandaliwa haukuwa na hata kipande kimoja cha nyama.

Upande wa mashtaka ulisema kwamba mshukiwa alitwaa upanga na kwanza akamkata Bi Mbuya kwa mguu wa kushoto chini ya goti na alipoanguka kwa uchungu, mshukiwa akatwaa kipande cha mbao na akamtwanga kwa kichwa, akamuua papo hapo.

Jaji Njuguna alisema kwamba ni lazima mshukiwa angeadhibiwa licha ya hali yake ya ulevi alipotekeleza mauaji hayo.

Aidha, jaji alisema wanakijiji walikuwa wamepinga kuachiliwa kwake wakimshuku kwamba angedhulu uthabiti na amani ya kijamii.

Katika hali hiyo, Nyaga sasa atakuwa radhi kuitisha nyama akiwa hapo jela kwa miaka 15 ijayo, na ikiwa atamudu, atakuwa huru akiwa na umri wa miaka 71.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Drama mzoga wa paka ukiondolewa dukani

Uhuru ahudhuria hafla ya maombi kwa waathiriwa wa...

T L