• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:02 PM
Anne Muratha apewa darasa baada ya kurushia watu keki

Anne Muratha apewa darasa baada ya kurushia watu keki

NA WANGU KANURI

WAKENYA mitandaoni wamelalamika baada ya mwanasiasa Anne Muratha, kunaswa kwenye video akiwarushia watu keki.

Anne ambaye anafahamika kwa jina Wamuratha alirushia umati keki katika hafla ya kusherehekea mwanahabari Njoroge Githinji kwa ufanisi aliopata katika miaka 16 akiwa kwenye tasnia ya uanahabari.

Hata hivyo, kufuatia video hiyo Wakenya wamezidondosha ghadhabu zao mitandaoni huku wengine wakimweleza sharti aombe msamaha.

“Wamuratha anawapa watu chakula kama kuku. Aki Wakikuyu shida yetu huwa wapi? Ni lini tulipoteza heshima yetu?” akauliza Mutemi Kiama.

“Kile Wamuratha alifanya kinawiana na kile wanawake wengi hufanya kwa kudhani vijakazi na walinda lango sio wanadamu. Tunapomshutumu Wamuratha angaza mwanamke wako,” akaandika Louis Vinnie.

“Lakini video hiyo ya Wamuratha akiwarushia wananchi wa Ruiru keki inahuzunisha. Hata watu maskini huchukuliwa kama watu wastaarabu na kuwekewa pilau mikononi. Chakula hakipaswi kurushwa vile!” akaandika Gathenya.

“Kile Wamuratha alifanya kinakaribiana na kile kilimfanya Kabogo kupoteza wadhifa wake kama gavana wa Kiambu. Wamuratha aombe msamaha au aadhibiwe na UDA. Wakenya si nguruwe wake,” akasema Thuo Githuku.

“Kwani Wamuratha hana wasaidizi wanaomsaidia katika kampeni zake? Anapaswa kuuliza Kabogo kilichomtendekea baada ya kuchukulia watu kama wanyama,” akaeleza Paul Ouma.

“Umetazama video ya Wamuratha ya jinsi anawachukulia wananchi wa kawaida? Kwani wanasiasa hutuchukulia vipi? Hii inavunja moyo sana kutazama,” akaandika Ian Mwai.

Wamuratha amelenga kuwania kiti cha mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Kiambu kupitia chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Naibu Rais William Ruto.

Hata hivyo, Wamuratha atamenyana na wanawake wengine 12 ambao pia wanamezea mate kiti hicho.

  • Tags

You can share this post!

Wakongwe 200 wapokea matibabu na chakula eneo la Mavoloni

Wito uchaguzi uwe wa amani Idd-ul-Fitr ikiadhimishwa nchini

T L