• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Wito uchaguzi uwe wa amani Idd-ul-Fitr ikiadhimishwa nchini

Wito uchaguzi uwe wa amani Idd-ul-Fitr ikiadhimishwa nchini

NA WAANDISHI WETU

WAISLAMU kote nchini jana waliadhimisha mwisho wa Ramadhan huku miito ikitolewa kwa Wakenya kudumisha utulivu na amani kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Kutoka Lamu, Mombasa hadi Kitale Waislamu walishukuru Mungu kwa kumaliza mfungo kwa amani.

Mjini Kitale katika Kaunti ya Trans Nzoia, maimamu waliwarai wanasiasa kuvumiliana, wakisema wanapaswa kujali mwelekeo wa nchi badala ya maslahi yao binafsi.

“Ni katika wakati huu ambapo hofu za ghasia za kisiasa huibuka. Matokeo yake huwa mapigano. Tunawaomba wanasiasa wetu kuzingatia amani wanapozunguka katika sehemu tofauti nchini kutafuta kura,” akasema Imam Mohamed Diko.

Aliyekuwa Mshirikishi Mkuu wa eneo la Bonde la Ufa, Bw George Natembeya, aliungana na Waislamu katika Msikiti wa Jamia na Pangani, ambapo aliahidi kuhakikisha kuwa changamoto zao zimeshughulikiwa.

Naibu Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu, Daniel Chemno, ambaye pia alijiunga na Waislamu, aliwarai Wakenya kuzingatia amani kote nchini.

“Tunakumbana na changamoto nyingi sana kama matumizi ya mihadarati, umaskini na uhalifu. Tunafaa kuungana ili kukabili changamoto hizi,” akasema Bw Chemno.

Tofauti na miaka iliyopita ambapo makundi tofauti ya Waislamu yaliadhimisha Idd-Ul-Fitr siku tofauti, shamrashamra za mwaka huu ziliandaliwa siku moja.

Hii ni baada ya Kadhi Mkuu, Ahmed Muhdhar kutangaza Jumapili usiku kwamba mwandamo wa mwezi ulionekana Witu, Tchundwa na Kipini, Kaunti ya Lamu.

“Ni jambo la kujivunia sana ambapo Waislamu wote wa Kenya walisherehekea pamoja kwa mara ya kwanza baada ya miaka kadhaa,” akasema Imam wa msikiti wa Sparki, Kaunti ya Mombasa, Sheikh Abu Hamza.

Imam huyo alisema kuwa kuna matumaini ya kuondoa mgawanyiko kuhusu kufunga na kufungua siku tofauti jinsi ilivyokuwa miaka iliyopita.

“Naona kutokana na Waislamu kusherehekea sikukuu kwa pamoja, kunaweza kuwa ni dalili nzuri ya suluhisho la kudumu la mgawanyiko uliokuwepo kumalizika ikiwa pande zilizokuwa zina tofauti zitakubaliana kuhusu jambo hilo,” akasema Sheikh Hamza.

Ripoti za Kalume Kazungu, Abdulrahman Sheriff, Alex Kalama Stanley Kimuge, Gerald Bwisa na Brian Ojamaa

  • Tags

You can share this post!

Anne Muratha apewa darasa baada ya kurushia watu keki

Sporty FC yajipatia miaka sita itinge Ligi Kuu ya Kenya

T L