• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 2:33 PM
Ashangaza kudai anafurahia seli baada ya kutekeleza mauaji

Ashangaza kudai anafurahia seli baada ya kutekeleza mauaji

NA TITUS OMINDE

MWANAMUME ambaye amekana kumuua mkewe na mwanawe wa miezi miwili aliambia mahakama ya Eldoret kwamba tangu wawili hao wauawe yeye hustarehe anapolala katika seli ya jela.

Alisema kuwa kamwe huwa hasumbuliwa na ndoto mbaya kutokana na tukio hilo.

“Sijawahi kukosa usingizi kwa madai ya kumuua mke wangu na mtoto wangu wa miezi miwili” Julius Kimutai mwenye umri wa miaka 31 aliambia mahakama kuu mjini Eldoret.

Mshtakiwa alisema hayo alipokuwa akihojiwa na wakili wa serikali Mark Mugun kuhusu mauaji ya kinyama ya wawili hao.

Bw Kimutai alisababish kicheko kortini chini ya Jaji Reuben Nyakundi alipodai kuwa hajawahi kusumbuliwa na ndoto mbaya na huenda mauaji hayo yalikuwa afueni kwake kupata usingizi mwanana.

“Hakuna wakati ambapo nimewahi kusumbuka usingizini kutokana na jinsi mke wangu na mtoto wa miezi miwili walivyofariki siku ya maafa ya Julai 2, 2017,” Kimuati alisema.

Bw Kimutai ambaye ni baba wa watoto wanne, alikuwa akihojiwa katika kesi ambapo anashtakiwa kwa kuwanyonga hadi kuwaua mkewe, Judith Jemaiyo na Abel Kipchirichir.

Mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Julai 2, 2017 katika kijiji cha Simotwo, Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Alishangaza mahakama alipokanusha taarifa yake iliyotiwa saini na polisi akisema kuwa hajui alichokuwa akitia saini kwani hajawahi kwenda shule.

“Ninakanusha kabisa kwamba nilitia saini taarifa hiyo mbele yangu katika kituo cha polisi. Hata sifahamu taarifa iliyo mbele yangu inayodaiwa kutiwa sahihi katika kituo cha polisi cha Iten,” aliteta Kimutai.

Jambo hilo lilimfanya wakili wa serikali kuomba mahakama kutoa agizo kwa Inspekta Mkuu aliyechunguza kesi hiyo kufika mahakamani na kutoa mwanga kuhusu suala hilo.

“Naomba tumuite ofisa mpelelezi ambaye ni mkaguzi mkuu, aje mahakamani na kutoa mwanga zaidi kuhusiana na kusainiwa kwa maelezo na mshtakiwa baada ya kukamatwa kutokana na mauaji ya mke wake na mtoto wa miezi miwili,” alisema Bw Mugun.

Mashahidi wanne wa upande wa mashtaka hadi sasa wametoa ushahidi wao katika kesi ya mauaji inayomkabili mshtakiwa.

Hakimu Nyakundi aliahirisha kesi hiyo kusikizwa baadaye, kwa maelekezo zaidi.

  • Tags

You can share this post!

Baba ashtaki binti yake kwa kumtusi

Matapeli wa magari kupitia NTSA waona cha mtema kuni

T L