• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 8:50 AM
Askari jela wakamatwa kwa kuingiza bangi gerezani

Askari jela wakamatwa kwa kuingiza bangi gerezani

MAKACHERO wakiongozwa na kinara wa Kitengo cha Kuchunguza Uhalifu wa Jinai eneo la Makadara, Bw Felix Nyamai Kithuku wanachunguza sakata ya bangi kuingizwa magerezani na askari jela.

Akiongea na Taifa Leo ofisini mwake mnamo Ijumaa, kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Makadara Bi Judith Nyongesa alisema askari jela hao tayari wamekamatwa.

Bi Nyongesa aliongeza kwamba wawili hao ni pamoja na konstebo na mwezake aliye na cheo cha sajini.

Isitoshe, walikamatwa na misokoto ya bangi 451 yenye thamani ya Sh11,000 bei ya mtaani.

“Askari hao walipatikana wamebeba misokoto 451 iliyofungwa kwa ustadi kiasi cha kutoshukiwa na mtu kirahisi. Mihadarati hiyo ilikuwa ya thamani ya zaidi ya Sh10,000 bei ya mtaani,” Bi Nyongesa akasema.

Bi Nyongesa aliongeza kwamba sakata hiyo imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu akihusisha kisa cha Ijumaa na tukio sawa na hili lililotokea mwaka 2022.

“Maafisa wengine walinaswa wakiingiza bangi katika gereza la Industrial Area. Maafisa wangu waliwakamata kabla ya kuingia katika lango la gereza wakati huo. Tuliwapeleka kortini na walifungwa kwa makosa hayo,” Bi Nyongesa akasema.

Kwa mujibu wa Bw Kithuku, wapelelezi walikuwa na habari kwamba bangi hiyo ingeingizwa jijini Nairobi ili kuchukuliwa na askari wa jela ndiposa iwafikie wafungwa ambao nao wangeiuza ndani ya jela.

Bw Kithuku alisema kitengo chake kikishirikiana na maafisa wake Bi Nyongesa kiliweka mikakati kabambe ili kufuatilia kisa chenyewe na kuweka mitego.

Wakifanya mipango yao, Bw Kithuku aliambia mwandishi wetu kwamba walijulisha utawala wa Jela ya Viwandani – Industrial Area (Nairobi Maximum Prison, Remand and Allocation) iliyoko mkabala wa barabara ya Enterprise katika eneo la Industrial Area kuhusu wanachochuguza.

“Mambo yalienda vizuri huku maafisa wangu maarufu undercover wakijipanga sawasawa tukiwa na wapelelezi waliokuwa wakiwafuata washukiwa wasiwagundue huku tukiwa na wengine wakiwasubiri katika lango la jela pasipokuwa na yeyote anayewatambua ndiposa washukiwa hao, ambao ni askari wa jela ya Viwandani waliviziwa mara moja wakipita lango kuu la jela wakibeba mzigo wao na ndipo walikamatwa,” Bw Kithuku akasema.

Aliongeza kwamba washukiwa wanachunguzwa zaidi na kuwasaidia polisi kuona kwamba wote wanaohusika na sakata hiyo wametiwa baroni.

“Kwa sasa, washukiwa wanazuiliwa kuhojiwa ili watupatie majina ya wale wanaowaletea mihadarati hiyo na wale ambao huiuza na tujue pia ni wapi inakokuzwa,” Bw Kithuku akaongeza.

Mapema 2022, askari wengine wawili walikamatwa wakiingiza bangi katika taasisi hiyo kwa njia sawa na ya Ijumaa.

  • Tags

You can share this post!

Pep asifia vijana kuwika mfululizo

TAHARIRI: Serikali sasa idumishe juhudi zake kukabiliana na...

T L