• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 7:05 PM
Jinsi Babu Owino alivyonusurika kutupwa jela kesi ya kumpiga risasi DJ Evolve

Jinsi Babu Owino alivyonusurika kutupwa jela kesi ya kumpiga risasi DJ Evolve

HABARI ZA HIVI PUNDE ZAIDI: Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma amesema leo Septemba 1 2023 kwamba atakata rufaa kwenye kesi hii -Mhariri

Na RICHARD MUNGUTI

MBUNGE wa Embakasi Mashariki, Paul Ongili Babu Owino aliponyoka kifungo cha jela mwaka mmoja Agosti 29, 2023 baada ya mahakama kumwachilia huru katika kesi ambapo alishtakiwa kumpiga risasi na kumjeruhi mtumbuizaji Felix Odhiambo Orinda almaarufu DJ Evolve miaka miwili iliyopita, lakini sasa huenda mashaka hayajamuondokea.

Ripoti kutoka afisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma amesema leo Septemba 1, 2023 kwamba anasubiri kuupata uamuzi huo ndipo akate rufaa katika Mahakama ya Rufaa.

Hii inamaanisha kwamba Mbunge huyo atahitaji kujinasua upya kutokana na kesi hiyo ambayo imekuwa kortini kwa miaka mitatu.

Mmano Jumanne, Hakimu Mkuu Mwandamizi mahakama ya Milimani, Bernard Ochoi alimwachilia huru Owino akisema “polisi walifanya uchunguzi duni katika kesi hiyo.”

Hata baada ya kuachiliwa huru, Owino aliahidi kortini ataendelea kumsaidia DJ Evolve kwa kugharamia matibabu yake hadi apone kabisa. DJ Evolve hawezi kutembea kutokana na jeraha alilopata shingoni mnamo Januari 17 2020.

Bw Owino alimweleza hakimu “nitaendelea kumsaidia DJ Evolve kupata matibabu hata nitaweka mipango kumpeleka DJ Evolve3 India kwa matibabu maalum.”

Bw Ochoi alisema kesi hiyo ilichunguzwa vibaya na masuala nyeti ambayo yangelishughulikiwa hayakugusiwa hata kidogo, kama vile bastola iliyompiga risasi DJ Evolve ilikuwa ya nani.

Pia, alisema polisi hawakueleza Owino alikuwa mlevi kiwango gani wakati wa kisa hicho.

Vile vile Bw Ochoi alisema uchunguzi wa kina haukufanywa.

Akimwachilia Bw Owino, hakimu alisema polisi hawakurekodi taarifa kutoka kwa DJ Evolve na ambaye “angelikuwa shahidi mkuu katika kesi hiyo na badala yake aliitwa na Owino kama shahidi wake na kusema hakupigwa risasi naye (Babu Owino).”

Pia alisema hawakuwa na uhasama wowote na mwanasiasa huyo.

Bw Ochoi alikashfu afisa wa polisi aliyechunguza kesi hiyo akisema alishindwa kutekeleza jukumu lake kwa kuchunguza kesi hiyo kwa njia inayofaa.

“Nimegudua kwamba afisa aliyechunguza kesi hii hakumpeleka Owino kupimwa kiwango cha pombe katika damu yake ili shtaka la kutokuwa na nidhamu na kutumia vibaya bastola yake lithibitishwe.”

Hakimu alisema kuna kasoro nyingi katika uchunguzi huo wa kushambuliwa kwa DJ Evolve.

“Sijui ikiwa afisa aliyechunguza kesi hiyo alizembea kazini mwake ama hajahitimu kuwa mchunguzi kamili. Kasoro nilizotambua katika kesi hii zikitokana na uchunguzi duni zimeniacha na maswali chungu nzima kuhusu utendakazi wa kikosi cha polisi,” alisema Bw Ochoi akimwachilia mbunge huyo.

Mahakama ilimpendekezea Mkurugenzi wa jinai siku za usoni kesi kama hii ichunguzwe na afisa wa cheo cha Inspekta.

Bw Ochoi alisema ni jambo la kusikitisha kuona polisi wakikosa kutenda kazi yao kwa njia ya ustadi.

“Afisa wa polisi aliyechunguza kesi hii dhidi ya Owino alitegemea video za kamera ya CCTV katika B Club badala ya kuwahoji kwa ufasaha waliokuwa katika kilabu hicho DJ Evolve alipojeruhiwa.

“Baada ya kutathmini ushahidi wote nimefikia uamuzi kwamba upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi dhidi ya Owino,” alisema Ochoi.

  • Tags

You can share this post!

Polisi wasubiri mshtakiwa ajisaidie wapate pete

Mwanamume ajitetea chang’aa ni ya kutakasa mke kwa...

T L