• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 10:55 AM
Corona yanusuru Sh290 milioni bungeni

Corona yanusuru Sh290 milioni bungeni

Na JOHN MUTUA

KANUNI kali za kupambana na ueneaji virusi vya corona kimataifa, ziliwezesha Kenya kuokoa zaidi ya Sh289.3 milioni kwa miezi mitatu ambazo kwa kawaida zingetumiwa na wabunge hasa kusafiri nje ya nchi.

Kiasi hicho cha pesa ambacho kilifichuliwa kwenye ripoti ya Mkaguzi wa Bajeti za Taifa (CoB), ni sawa na kuhifadhi takriban Sh3.2 milioni kila siku.

“Baadhi ya matumizi ya bajeti yalipungua, na hili lilitokana na athari za kanuni za kupambana na Covid-19 ambazo zilipitishwa na serikali kuzuia ueneaji wa ugonjwa huo,” Mkaguzi wa Bajeti, Bi Margaret Nyakang’o akasema kwenye ripoti hiyo.

“Matumizi hayo yalijumuisha ya usafiri, mafunzo na kuwahudumia wageni bungeni ambayo huwa ni kiasi kikubwa katika matumizi ya fedha ya idara za serikali,” akaeleza.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo inayohusu matumizi ya fedha kati ya Julai na Septemba mwaka huu, wabunge walitumia Sh966.3 milioni kwa usafiri, kupokea mafunzo na marupurupu ya kikazi. Kiwango hicho kilipungua ikilinganishwa na mwaka uliopita, ambapo Sh1.255 bilioni zilitumiwa kwa kipindi sawa na hicho.

Katika kipindi hicho mwaka huu, wabunge walitumia Sh16.88 milioni kwa usafiri nje ya nchi, kiasi ambacho kilipungua mno kutoka Sh349.3 milioni ilivyokuwa mwaka uliopita.

Inaaminika hali hii ilisababishwa na jinsi mataifa mengi ulimwenguni yaliweka vikwazo vya usafiri ndani na nje ya nchi kwa muda mrefu tangu maambukizi ya virusi vya corona yalipotangazwa kuwa janga kimataifa.

Kiasi cha fedha kilichotumiwa kwa mafunzo ni Sh4.14 milioni, ambacho kilipungua kwa asilimia 82 ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka uliotangulia.

Wabunge hupokea Sh5,000 za marupurupu kuhudhuria vikao vya kamati za bunge, ambapo wenyekiti hupokea Sh8,000. Vile vile, wao hulipwa marupurupu ya Sh18,000 kwa siku wanapohudhuria mikutano katika miji mikubwa kama vile Mombasa na Kisumu, na Sh10,500 katika miji midogo.

Hata hivyo, takwimu za CoB zinaonyesha kuwa, marupurupu ya wabunge kusafiri ndani ya nchi pamoja na ya kufanya kazi usiku yaliongezeka. Spika wa Bunge la Taifa, Bw Justin Muturi, alisitisha vikao vya kamati isipokuwa vinavyohusu masuala ya bajeti na afya.

Bw Muturi pia aliagiza kupunguzwa kwa idadi ya wabunge wanaohudhuria vikao bungeni hadi 50, akaagiza kwamba warsha zote ziwe zikifanywa katika majengo ya bunge Nairobi.

Kwa miaka mingi, wabunge wamekuwa wakikashifiwa na baadhi ya wananchi na mashirika ya kijamii kwa kutumia fedha nyingi kwa masuala ambayo hayana umuhimu kwa umma.

Miongoni mwao ni safari za nchi za kigeni ambazo huonekana hazileti faida kwa mwananchi wa kawaida. Wabunge pia hukosolewa kwa kupokea marupurupu kuhudhuria vikao, ilhali hilo ni mojawapo ya majukumu yao ambayo wanalipiwa mishahara minono.

You can share this post!

Uhuru atoa amri miradi Kisumu ikamilike upesi

Ugaidi Lamu ulipungua 2020