• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 3:46 PM
Daktari wa KNH aliyejiua kuzikwa habari zaidi zikiibuka

Daktari wa KNH aliyejiua kuzikwa habari zaidi zikiibuka

Na MARY WANGARI

DAKTARI wa Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) aliyedaiwa kujitoa Uhai, Dkt Lydia Kanyoro atazikwa Jumamosi, June 19 nyumbani kwao katika kijiji cha Iguriini, Kaunti ya Kirinyaga.

Haya yanajiri wakati makachero kutoka Kituo cha Polisi cha Milimani, wameanzisha uchunguzi kufichua kiini hasa cha kifo cha daktari huyo huku habari za kina zikiibuka.

Bi Kanyoro, 35, alikuwa akihudumu kama daktari wa watoto na ni upendo wake na kujitolea katika kazi yake kulikofanya familia na marafiki zake kumbandika jina la “Baby Doc.”

Kabla ya kifo chake katika hali ya kutatanisha, daktari huyo alikuwa akisomea Shahada ya Uzamili kuhusu Sayansi ya Afya katika Kituo cha Chuo Kikuu cha Nairobi, KNH.

Hata hivyo, kulingana na jumbe kadhaa alizochapisha katika akaunti zake mitandaoni, yamkini afisa huyo wa afya alikuwa anaandamwa na msongo wa mawazo ikiwemo matatizo ya kikazi na kuhofia maisha yake.

Matatizo ya kimawazo pamoja na vifo vya watoto watatu aliokuwa akitibu huenda yalimkatiza tamaa ya kuishi na kumfanya kujitia kitanzi kwa kujidunga dozi hatari za dawa.

“Kazi inaniua… Nimelazimika kufunga matumbo ya watu kwa kutumia mwangaza wa tochi au adhuhuri moja nilipolazimika kuacha watoto watatu kuaga dunia kwa sababu sikuwa na nilichohitaji kuwaokoa,” alisema Bi Kanyoro kupitia ujumbe mmoja mtandaoni.

Madaktari wenzake walimtaja mwendazake kama daktari mwenye maarifa makuu ambaye kujitolea kwake kuhusu wagonjwa wake hakukuwa na kifani.

Dkt Kanyoro alikuwa akitafiti kuhusu matibabu ya hewa ya oksijeni kwa wagonjwa wa cCovid-19, kulingana na daktari mwenzake, Mercy Korir.

“Kazi yake na kujitolea kwake kuhusu wagonjwa wake kulikuwa bayana. Madaktari wenzake, wafanyakazu na walimu wote wanasema jambo hilo hilo. Lydia alikuwa mwerevu sana,”

“Miongoni mwa tafiti zake za mwisho ilikuwa kuhusu matumizi ya Oksijeni kutibu wagonjwa wa Covid-19. Hii ilikuwa kupitia kongamano kielektroniki mnamo Aprili 2021. Alijadili kuhusu maski za Venturi na oksijeni kwa ukakamavu mkuu kana kwamba alikuwa amezitumia,” alisema Dkt Korir.

Kulingana na polisi, Bi Kanyoro alifika katika ukumbi wa mhadhara saa tatu na kujisajilisha kabla ya kuondoka nusu dakika baadaye na kuelekea maegeshoni kwenye gari lake.

Walisema kuwa mwendazake aliwapigia simu baadhi ya jamaa zake na kuwafahamisha alichokusudia kufanya na watakapopata mwili wake kabla ya kujidunga sindano iliyosheheni dawa hatari kabla ya kukata roho.

Kulingana na polisi mwili wa marehemu ulipatikana saa saba adhuhuri kwenye kiti cha nyuma cha gari lake pamoja na chupa za dawa hizo na kijibarua alichoacha.

  • Tags

You can share this post!

Raila akanyagia ‘tosha’ ya urithi wa Joho

KENYA IMESOTA!