• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Delmonte yawapiga jeki wasichana wa Mwana Wikio kwa kuwapa sodo

Delmonte yawapiga jeki wasichana wa Mwana Wikio kwa kuwapa sodo

Na LAWRENCE ONGARO

WANAFUNZI wa kike wa Shule ya Upili ya Mseto ya Mwana Wikio katika Kaunti ya Murang’a wamepokea sodo za kuwafaa wakati wa hedhi.

Kampuni ya Delmonte ilishirikiana na Chania Cleaners, Cortex, Salam Ltd, na Mobias Motors kuhakikisha wanafunzi wanapata bidhaa hiyo muhimu kwa usafi.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi Hilda Mwangi, alishukuru kampuni ya Delmonte kwa kujitokeza wazi kuona ya kwamba wanafunzi wa kike wanasaidiwa kupata sodo za bure.

“Tunaelewa kuwa wanafunzi wengi wanatoka katika familia zisizojiweza kifedha na kwa hivyo wanafunzi hao wanapitia changamoto ya kukosa sodo za kujikimu,” alisema Bi  Mwangi.

Alisema wao kama walimu wanashuhudia kila mara wanafunzi wa kike wakikosa kuhudhuria vipindi vya masomo darasani hasa wakati wakiwa kwenye hedhi.

“Jambo hilo limekuwa likituchanganya huku pia wazazi wakikosa la kutuambia,” alisikitika mwalimu huyo mkuu.

Mbali na sodo, wanafunzi pia walipata sabuni na karatasi shashi.

“Tutazidi kushirikiana na kampuni hiyo ili kuwa na ushirikiano wa karibu na kuweza kunufaika kutokana na miradi tofauti,” alisema mwalimu mkuu.

Meneja wa ajira katika kampuni ya Delmonte Bw Gerald Matoke alisema kampuni hiyo imeanza mpango wa kusambaza sodo katika shule tofauti huku wakilenga zaidi ya wasichana 10,000.

“Kampuni ya Delmonte imeanza kuzuru shule za Murang’a na Kiambu ili kufikia wasichana na kuwapa sodo,” alisema Bw Matoke.

Alisema watafikia pia wanawake katika maeneo hayo na watawapa sodo za bure.

Msanii Arvil Nyambura alitoa wito kwa serikali kuondoa ushuru kwa sodo na badala yake izisambaza bila malipo ili kila msichana apate bila shida. Aliwashauri wanafunzi wa Mwana Wikio wafanye bidii masomoni ili maisha yao yaimarike hapo baadaye.

Mchekeshaji maarufu wa kipindi cha Churchill Show, Bw Jasper Muthomi, alitoa wito kwa serikali kuondoa ushuru wa sodo ili wasichana waweze kuzinunua kwa bei nafuu.

Afisa wa uhusiano mwema wa  kampuni ya Delmonte, Jackline Muthoni, alisema kampuni hiyo imeanza ushirikiano wa karibu na wananchi hasa kutoka mashinani kwa kuzindua miradi tofauti.

Alisema kwa sababu kampuni hiyo ni ya kimataifa itazuru maeneo yote ya nchi.

Hadi kufikia sasa, kampuni hiyo imesaidia wasichana wapatao 1,500.

“Huo ni mwanzo tu lakini bado tunalenga kuzindua miradi mingi katika maeneo tofauti nchini,” alisema afisa huyo.

Alisema kampuni hiyo imeanza kujitolea kuona ya kwamba inafaa umma kwa kujihusisha na maswala tofauti ya kijamii.

  • Tags

You can share this post!

Atakayechukua nafasi ya Sabina Chege kutajwa katika PG ya...

Makundi ya kidini Kenya yasifu Rais Museveni kuharamisha...

T L