• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 5:47 AM
Eric Omondi aomboleza kupoteza mtoto aliyetaka kusaidia atibiwe nguvu za umeme zilipopotea

Eric Omondi aomboleza kupoteza mtoto aliyetaka kusaidia atibiwe nguvu za umeme zilipopotea

NA SAMMY WAWERU

MCHEKESHAJI Eric Omondi anaomboleza kupoteza mtoto aliyetaka kumsaidia kupata matibabu, baada ya nguvu za umeme kupotea nchini mnamo Ijumaa, Agosti 25, 2023.

Ijumaa hiyo jioni, maeneo mengi nchini stima zilipotea na kusababisha hasara hasa kwa huduma za kimatibabu, mikahawa na wafanyabiashara wanaotegemea nguvu za umeme.

Kulingana na Omondi, alipaswa kuchangisha pesa kupitia harambee ya mbashara Facebook za wagonjwa waliotarajiwa kuenda ng’ambo kupata matibabu.

Mmoja wa wagonjwa hao, ni msichana mwenye umri wa miaka 9 ambaye kulingana na msanii huyo alitarajiwa kusafiri India kufanyiwa upasuaji wa figo.

Hata hivyo, kwa sababu ya stima kupotea alimpoteza – kuaga dunia.

Akielezea masikitiko yake, Omondi alisema waliohusika kusababisha kupotea kwa nguvu za umeme wanapaswa “kubeba mzigo wa matendo yao”.

“Ni huzuni kupoteza msichana mwenye umri wa miaka 9 ambaye alipaswa kusafiri India kufanyiwa upasuaji wa figo. Nilikuwa nifanye mchango kupitia Facebook (Facebook Live), lakini kwa sababu ya stima kupotea sikuweza. Waliohusika lazima wabebe huo mzigo,” mcheshi huyo alielezea kupitia video aliyopakia katika ukurasa wake rasmi wa Facebook.

Aidha, Omondi alisema alikuwa na orodha ya wagonjwa aliopaswa kuchangia hela ila haikuwezekana.

Alisema, “Endapo tutapoteza wagonjwa ambao nilikuwa niwafanyie harambee kukusanya pesa za matibabu India ambazo sikufanikiwa, waliohusika lazima walipie. Ikiwa hawatalipia, kazi zao hazitadumu.”

Kando na adhabu kisheria, msanii huyo anataka wagonjwa wake walipiwe tiketi za ndege kuenda ng’ambo kutibiwa.

Stima zilipotea kwa zaidi ya saa 12, na hata baada ya hali kurejea kama kawaida utendakazi katika Kampuni ya Kusambaza Nguvu za Umeme Nchini, Kenya Power, serikali haikuchukua hatua yoyote.

Badala yake, Wizara ya Uchukuzi ilifanya mabadiliko katika Halmashauri ya Huduma za Ndege Nchini (KAA) ambapo Mkurugenzi Mkuu, Alex Gitari alifutwa kazi kufuatia kutatizika kwa huduma katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi.

Nafasi yake ikitwaliwa na Henry Ogoye kama Kaimu Mkurugenzi, ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa msimamizi Mipango ya Ushirika KAA, sababu za Bw Gitari kutimuliwa zilitajwa kama kukosa kushughulikia jenereta za JKIA ili huduma ziendelee kama kawaida.

Biashara nyingi zilikadiria hasara kutokana na tukio hilo, ambalo Kenya Power inahoji ilitokana na hitilafu – linalosalia kutoeleweka kufikia sasa.

Kwa upande wake Eric Omondi, sharti serikali itoe adhabu la sivyo visa vya aina hiyo vitazidi kushuhudiwa.

“Ingekuwa nchi za ng’ambo, kuna watu ambao wangekuwa wamejiuzulu.”

  • Tags

You can share this post!

Maswali yaibuka kuhusu Gachagua kudhalilisha majadiliano...

Tanzania yailemea Kenya katika uvutaji bangi – Utafiti

T L