• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Familia 3,000 zaagizwa kuhama Mto Ngong

Familia 3,000 zaagizwa kuhama Mto Ngong

Na SAMMY KIMATU

ZAIDI ya familia 3,000 zinazoishi karibu na mto Ngong kwenye tarafa ya South B, kaunti ndogo ya Starehe ilioko katika Kaunti ya Nairobi wameamriwa na serikali kuondoka kutoka kwa nyumba zao mara moja.

Aidha, wameshauriwa kuhamia maeneo yaliyo salama ili kuepukana na mafuriko msimu huu wa mvua ya mwezi Aprili.

Agizo hilo lilitolewa na serikali kupitia kwa chifu wa eneo hilo, Bw Charles Mwatha.

Katika ujumbe wake, Bw Mwatha alisema kila mwaka, hasa msimu wa mvua ya kati ya mwezi Machi na Aprili, serikali huagiza watu wake kuhamia maeneo yaliyo salama ili kuepuka maafa na uharibifu wa mali kutokana na athari za mafuriko.

‘’Huwa tunatoa tahadhari za mapema kila mwaka kabla ya mwezi Machi na Aprili ndiposa wahamie maeneo salama kabla ya kingo za mto Ngong kufurika na maji kuingia katika nyumba zao,’’ Chifu Mwatha aliambia wanahabari.

Aliongeza kwamba wanaoathirika zaidi huwa wakazi katika mtaa wa mabanda wa Maasai Village, Hazina, Sokoni na Fuata Nyayo.

Katika lokesheni ya Landi Mawe, chifu wa Eneo hilo, Bw Kikuvi Mulandi alisema wakazi katika mtaa wa mabanda wa Kaiyaba, Kenya Wine, Kikaloni, Mandazi Roada na wanaoishi katika eneo la Bundalangi nao wahamie kwenye miinuko ili wakijinge dhidi ya mafuriko.

“Katika Landi Mawe familia zaidi ya 1,000 watalazimika kuhamia maeneo yaliyo juu ili wasiathirike kutokana mafuriko yanayotarajiwa mwaka huu,’’ Bw Mulandi asema.

Mwaka jana, familia zilizoathirika zilitengewa uwanja wa shule ya Msingi ya Mariakani, uga wa palipokuwa kituo cha Goal Kenya na katika makanisa kadhaa kwenye tarafa ya South B kuwa kambi ya muda.

Vilevile, wakiwa kwenye kambi hizo, waathiriwa hupokea misaada ya serikali, mashirika, makanisa na wahisani wengine ikiwemo vyakula, mavazi, vinywaji, vyandarua vya kuzuia mbu miongoni jwa usaidizi mwingine.

Kando na nyumba, vibanda vya biashara ya kuuza vyakula, vioski, saluni na shule nne huathirika pia.

Miongoni mwa shule ambazo wanafunzi hulazimika kukaa nyumbani ni pamoja na Brightstar Academy, Shule ya Upili ya Brightstar, Shule ya Upili ya Viwandani na Shule ya Msingi ya St Elizabeth zote zikiwa katika kaunti ndogo ya Makadara.

Kwa mwaka wa tatu mfululizo, katika shule ya Msingi ya St Elizabeth ilioko mtaani wa mabanda wa Lunga Lunga, maji hufika kina cha futi nne huku kila darasa, stoo na ofisi zikijaa maji.

“Huwa tunalazimka kurudisha watoto nyumbani baada ya maji kuleta balaa shuleni na kuvuruga masomo,’’ akasema mkurugenzi Mkuu wa Mukuru Promotion Centre (MPC) Mtawa Mary Killeen. MPC ni mfadhili mkuu wa baadhi za shule za huma tarafani South B na Viwandani.

Mtawa Killeen aliongeza kwamba sababu moja ya mafuriko hayo huchangiwa na wanyakuzi wa ardhi walionyakua kingo za mto na kujenga nyumba za kukodisha huku wakibana mto.

Ofisa mmoja wa mazingira kutoka kaunti ndogo ya Starehe alisema utafiti umeonyesha mto ‘umenyongwa’ baada ya kuwa mwembamba kutokana na ujenzi wa nyumba pande zote na kufungia maji njia ya kupitia.

“Wakazi pia hutupa taka ndani ya mto na kusababisha daraja la Hazina/Kaiyaba kuziba na kuwa halipitiki. Wanaotumia daraja hili kuunganisha South B na barabara ya Entreprise kuingia Eneo la Viwanda hulazimka kutumia njia badala kuendesha pikipiki na magari,’’ Bw Christopher Lunalo Mandevu akasema.

Takataka inapoziba daraja, vijana hujitolea kuzibua japo kwa ada kiasi kutoka kwa waendeshaji magari.

You can share this post!

Mreno aliyetuma droni kwa makazi ya Ruto ashtakiwa

Wakazi walia barabara mbovu zinawaletea hasara