• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 PM
Familia yalilia haki baada ya jamaa kuuawa, kakake kujeruhiwa walipohudhuria disko matanga

Familia yalilia haki baada ya jamaa kuuawa, kakake kujeruhiwa walipohudhuria disko matanga

Na KASSIM ADINASI

Familia moja eneo la Umala, Ugunja, Kaunti ya Siaya inalilia haki baada ya jamaa yao kuuawa na kakake kupatwa akiwa hana fahamu baada ya kuhudhuria hafla ya disko matanga.

Usiku wa Jumanne, Septemba 5, 2023, Jared Ongoro, 40, na kakake mdogo Obuori Ongoro waliondoka nyumbani kwenda kwa maombolezo ya usiku, yanayojulikana maarufu kama disko matanga, katika kijiji jirani cha Siranga, Siaya.

Hiyo ikawa mara ya mwisho ya wawili hao kuonekana pamoja.

Asubuhi iliyofuata, mwili wa Jared ulipatikana umetupwa kando kando ya Mto Nzoia huku kakake akipatikana hana fahamu karibu yake.

Alipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Siaya ambapo anaendelea kupokea matibabu huku mwili wa Jared ikipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti ukisubiri upasuaji kubaini chanzo cha kifo chake.

Lakini wiki nzima baadaye, hakuna upasuaji uliofanywa wala yeyote kutiwa mbaroni na polisi, jambo lililofanya familia kuanza kushuku kwamba kuna kasoro.

Wakizungumza na Taifa Dijitali, Johannes Owino, binamu ya mwendazake alisema kwamba hakujakuwa na juhudi za kunasa waliohusika na kisa hicho.

“Ni wiki sasa tangu kisa hiki ambacho kiliacha jamaa yetu amefariki kitokee, na hakuna chochote kinachoendelea. Hakuna upasuaji wala juhudi zinazoweza kuonekana za kunasa waliotekeleza unyama huu,” akalalama Bw Owino.

Wasiwasi wa familia ni kuhusu siku ambayo upasuaji utafanywa na serikali kama inavyohitajika kisheria huku kukiwa tayari kushatoka idhini ya kuzika mwili huo.

Bw Owino analaumu polisi katika kituo cha Umina kwa kukosa kuwasili kujibu vilio vya kuhitaji usaidizi.

“Usalama katika lokesheni ndogo ya Umala hairidhishi na hali imekuwa hivi kwa muda sasa. Maafisa katika kituo hicho cha polisi hawatoi usaidizi wowote,” akaongeza.

Alimuomba Mkuu wa Polisi katika Kaunti ya Siaya Michael Muchiri awape uhamisho maafisa hao na kuleta ‘wachapa kazi’ katika eneo hilo.

“Polisi katika kituo cha Umina huwa wepesi sana wanapokamata wanawake wanaopika pombe za kienyeji, lakini wanapoitwa kusaidia wakazi wanapovamiwa na wahalifu huwa hawaonekani. Tunaomba wabadilishwe ili waletwe wale wanaojua majukumu yao,” akasema.

Marehemu ameacha watoto wanne.

Majeruhi, Bw Obuori angali katika hali mahututi hospitalini.

Kamanda wa polisi wa Kaunti Ndogo ya Ugenya Benard Wamugunda aliambia Taifa Dijitali kwamba kisa hicho kinashughulikiwa na kitengo cha Upelelezi wa Jinai (DCI) na kwamba hivi karibuni watanasa washukiwa.

Kuhusu kufanyia mwili upasuaji, afisa huyo alihakikishia familia kwamba shughuli zote zitafanywa.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Huenda nyama ya pundamilia inauzwa madukani kupitia mlango...

Wanaotumia bangi Kenya wameongezeka pakubwa katika miaka...

T L