• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Wanaotumia bangi Kenya wameongezeka pakubwa katika miaka mitano – Nacada

Wanaotumia bangi Kenya wameongezeka pakubwa katika miaka mitano – Nacada

Na MERCY CHELANGAT

IDADI ya Wakenya wanaotumia dawa za kulevya, ikiwemo bangi, inazidi kuongezeka na kusababisha matatizo ya akili kama vile kiwewe miongoni mwa wanaozitumia, ripoti ya utafiti wa Mamlaka ya Taifa ya Kukabiliana na Pombe na Dawa za Kulevya (NACADA) inasema.

Utafiti wa Mamlaka hiyo unatoa taswira ya nchi iliyo katika hatari ya kutumbukia katika ulevi na matumizi ya dawa za kulevya, iwapo mikakati haitawekwa kukabiliana na hali hii.

“Idadi ya watu ambao kwa wakati huu wanatumia bangi imeongezeka kwa asilimia 90 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Eneo la Nairobi lina idadi kubwa zaidi ya watu wanaotumia bangi kwa wakati huu (asilimia 6.3) ikifuatwa na Nyanza (asilimia 2.4) na Pwani (asilimia 1.9) kwa mujibu wa utafiti wa NACADA.

Shirika hilo linahusisha ongezeko hili na nadharia kwamba bangi haina madhara kwa afya.

Matumizi mabaya ya dawa zinazopaswa kutumiwa kwa ushauri wa daktari pia yamekuwa donda ndugu huku wengi wakiendelea kutekwa na uraibu huo. Dawa hizi zinazofahamika kwa lugha ya mtaa kama “mchele” zimekuwa zikisababisha madhara kwa wanaozitumia.

Uraibu wa dawa hizi umekuwa tatizo hasa miongoni mwa vijana hasa eneo la pwani. Wahalifu pia wamekuwa wakizitumia kulewesha watu kabla ya kuwaibia mali yao.

Utafiti wa Mamlaka hiyo ulibaini kwamba watu 494,218 wanachanganya dawa tofauti za kulevya na kwamba watu1 504,377 walio na umri wa kati ya miaka 22 na 35 wanatumia aina moja ya dawa za kulevya.

Utafiti wa NACADA ulifichua kwamba pombe ndicho kileo kinachotumiwa vibaya kwa wingi nchini Kenya hasa chang’aa, pombe za kienyeji na zinazouzwa kwa chumba ndogo zinazoweza kubebwa kwa urahisi.

Utafiti unasema kuna ushahidi wa watoto kutambulishwa kwa matumizi ya vileo wakiwa na umri mdogo.
“Utafiti ulipata ushahidi wa matumizi ya vileo miongoni mwa watoto licha ya athari hasi za kuanza kuvitumia mapema,” inasema sehemu ya utafiti.

Baadhi ya vileo hivyo zikiwemo dawa za kulevya huwa zinauzwa katika mtandao na hii ni changamoto katika kuthibiti matumizi yake.

NACADA inasema kwamba matumizi ya dawa za kulevya na vileo imesababishia raia wengi mfadhaiko miongoni mwa matatizo mengine ya akili.

“Mmoja kati ya Wakenya watatu walio na umri wa kati ya miaka 15 – 65 years (8,390,616) alikuwa na kiwango kidogo cha mfadhaiko. Hatari ya mafadhaiko miongoni mwa watumiaji wa pombe ilikuwa mara 2.3 juu ikilinganishwa na wasioitumia,” utafiti unaeleza.

NACADA inasema katika utafiti huo kwamba maeneo ya Kati, Nairobi na Mashariki yalikuwa na ongezeko la baa katika miaka mitano iliyopita huku maeneo ya Nairobi, Nyanza na Kati yakiwa na ongezeko la watoto wanaokunywa pombe.

Utafiti unasema mbali na bangi na pombe, utafunaji wa miraa, uvutaji wa sigara na tumbaku zimeongezeka miongoni mwa Wakenya wa kuanzia umri wa miaka 15 na 65.

  • Tags

You can share this post!

Familia yalilia haki baada ya jamaa kuuawa, kakake...

Hatutabebwa na ‘tam tam’ za Ruto, magavana wahakikishia...

T L