• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
Familia zaidi ya 1,000 zilizoathirika na moto kusubiri zaidi kabla ya kurudi nyumbani

Familia zaidi ya 1,000 zilizoathirika na moto kusubiri zaidi kabla ya kurudi nyumbani

NA SAMMY KIMATU

FAMILIA zaidi ya 1,000 zilizoathirika katika mkasa wa moto katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Maasai, kaunti ndogo ya Starehe bado zitasubiri zaidi kurudi kwa makao yao.

Naibu Kamishna katika kaunti ndogo ya Starehe, Bw John Kisang ameambia Taifa Leo kwamba serikali ilikuwa na utaratibu wa kufuatwa kabla ya nyumba kujengwa upya.

“Serikali haingeruhusu wakazi kurudi makwao kiholela. Kamati husika zikiongozwa na mkuu wa tarafa na machifu walihakikisha barabara zinatengwa ili kutumiwa wakati wa dharura,” Bw Kisang akasema.

Bw Kisang aliongeza kwamba vibanda vilivyoziba njia iliyoratibiwa awali viliondolewa na wenyeji kuonywa dhidi ya kufunga barabara inayopakana na ua unaotenganisha Mtaa wa Mukuru-Maasai na mtaa wa Hazina.

Kwa wakati huu, waathiriwa huishi kwa marafiki, jamaa zao na wengine kubahatika kuhamia mitaa mingine ilio karibu.

Kisa hicho cha moto kilitokea Mnamo Januari 2023. Aidha nyumba zaidi ya 300 ziliteketea kando na vibanda vya biashara.

Kiongozi wa wanawake katika eneo la Hazina, Bi Mary Kiminza Charles alisema wauguzi katika ambulensi ya Shirika la Msalaba Mwekundu Nchini walihudumia watu tisa waliopata majeraha wakati wa kukurukakara za kuzima moto.

“Wauguzi katika ambulensi walihudumia watu tisa ilhali mtu wa kumi alipata majeraha mabaya kichwani aliposhukiwa kuwa mporaji. Alikimbizwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH),” Bi Charles akaambia Taifa Leo.

Mkuu wa polisi eneo la Makadara, Bi Judith Nyongesa alisema ofisi ya DCIO inachuguza kisa hicho kubaini chanzo cha moto huo.

  • Tags

You can share this post!

Usokotaji manyoya wapiga jeki kina mama wa Kibra

Papa Francis aanza ziara yake rasmi Afrika

T L