• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:50 AM
Usokotaji manyoya wapiga jeki kina mama wa Kibra

Usokotaji manyoya wapiga jeki kina mama wa Kibra

NA LABAAN SHABAAN

KIKUNDI cha kina mama kwa jina Ayani eneobunge la Kibra, Kaunti ya Nairobi kimedumu zaidi ya miongo mitatu tangu kuasisiwa kuunda bidhaa mbalimbali kutoka kwa manyoya ya kondoo na pamba.

Ni kundi ambalo lilianza mwaka wa 1986 kama chama cha wanawake walioshindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya matatizo ya kiuchumi. Walipoanza, walikuwa wanawake 32 lakini sasa wamebakia 8.

Kati ya changamoto wanazopitia ni mgogoro baina ya wanachama; wengine wanataka wauze mali ya kundi hili na kugawana pesa kila mmoja aende zake.

Hadi sasa hawajafikia mwafaka huu kwa sababu viongozi wanaamini mustakabali wao ungali angavu.

Mmoja wa viongozi wa kundi hili, Jira Musembi anasikitikia maendeleo ya chama kilichonawiri awali kuwanogeshea maisha akikadiria mali ya kundi kuwa zaidi ya Sh20 milioni.

Mwenyekiti wa kundi hili Lucy Wairimu, 52, anasema walianza kwa kuchanga Sh20 kila mmoja na baadaye wakapokea ufadhili kutoka kwa wahisani wa Japan waliowafunza stadi za kushona nguo na kusokota manyoya ya kondoo kuunda nyuzi.

“Tulipewa ruzuku na wahisani pamoja na ujuzi na vifaa vya kushona. Kutokana na fedha tulizopokea, tulijenga makao yetu ambapo tunafanyia kazi hii,” Wairimu anaambia Akilimali.

Miongoni mwa vitu wanavyounda ni mazulia, nyuzi, mikeka, fulana, skafu, kofia, vitambaa na aina tofauti za mavazi ambayo huuzwa kwa kati ya Sh500 na zaidi ya Sh5,000.

Aghalabu kina mama wa Ayani hununua manyoya ya kondoo kutoka kwa wafugaji wa kondoo Kaunti ya Nakuru ambapo kilo moja ya manyoya huuzwa kwa kati ya Sh200 na 300 kutegemea na ubora.

“Kwa sasa sisi hununua manyonya ya kondoo kilo 150 kila wiki lakini kitambo tulinunua kwa wingi sana hadi uchumi ulipoharibika,” mwenyekiti wa Ayani anaeleza.

Katika karakana yao iliyo kwenye ardhi thumni ya ekari, kuna vyumba zaidi ya vitano vyenye majukumu mbalimbali; stoo, darasa, maonyesho na eneo la kazi.

“Tunafanya kazi hii kwa mkono kutumia vifaa vya juakali. Pengine ni kwa sababu tuko mashinani hatuonekani ama serikali imetupuuza; tunafaa kuwa tunatumia mashini kufikia sasa na kuwa mbali sana kimaendeleo,” Wairimu anasikitika.

Katika kipindi cha mlipuko wa janga la corona, biashara yao ilidorora kwa muda hadi karibu wafunge milango lakini walivumilia na kuwa wakakamavu kusimama imara.

Upo wakati walikodisha sehemu ya nyumba zao kwa wamiliki wa shule za chekechea. Hawakukodisha sana kwa sababu walipigwa na dhoruba ya uchumi kwa sababu ya kanuni kali za kudhibiti corona zilizoathiri vitega uchumi.

Licha ya changamoto walizopitia Wairimu anafurahia kuwa kazi hii imesaidia kusomesha watoto wao na kukidhi mahitaji ya familia yao kwa muda mrefu.

Mbali na kuuza bidhaa wanazotengeneza, kundi la Ayani kadhalika hutoa mafunzo kwa vijana wa mtaa wa Kibra wenye nia ya kupata stadi hii na kujianzishia kazi zao.

“Tunaomba serikali kutusaidia kuimarisha kituo hiki kuwa asasi ya mafunzo inayotambulika ili kuvutia wanafunzi na kusaidia jamii,” Wairimu anaomba.

Bidhaa wanazounda husambazwa kwa wauzaji wengine wanaonunua kwa bei ya jumla lakini pia wateja huja na kununua kutoka kwao.

Kina mama hawa wanakiri kuwa, yamkini kutochangamkia mitandao ya kijamii katika mauzo kumewaathiri kibiashara kwa sababu wanahisi karne ya sasa inahitaji biashara kwenda sambamba na utandawazi.

Kina mama wa Ayani wangali na matumaini kuwa watakata utepe wa ushindi wakizidi kujikakamua na kuomba msaada wa wahisani na serikali.

  • Tags

You can share this post!

TUJIFUNZE UFUGAJI: Weka sheria kudhibiti wanaoingia kwenye...

Familia zaidi ya 1,000 zilizoathirika na moto kusubiri...

T L