• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Ford Kenya yakanusha kufanya mazungumzo ya 2022 na Dkt Ruto

Ford Kenya yakanusha kufanya mazungumzo ya 2022 na Dkt Ruto

Na ONYANGO K’ONYANGO

VIONGOZI wa chama cha Ford Kenya wamekanusha madai kwamba, wanafanya mazungumzo ya siri na Naibu Rais William Ruto ili kuunda muungano kabla ya Uchaguzi Mkuu 2022.

Naibu Kiongozi Richard Onyonka, ambaye pia ni mbunge wa Kitutu Chache, aliambia Taifa Leo kuwa chama chao kinaamini maono ya muungano wa One Kenya Alliance (OKA).

“Taarifa zinazoenea kwamba tunazungumza na Naibu wa Rais ili kuunda muungano, si ya kweli. Kwa sasa tunaamini muungano wa OKA.

“Msimamo wetu ni kwamba kiongozi wa chama ni sharti aidhinishwe na chama kabla kufanya mazungumzo ya kuunda miungano. Hajawahi kuja kwetu kutushauri,” akasema Bw Onyonka.

Muungano wa OKA unajumuisha kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi (ANC), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Gideon Moi wa Kanu.

Bw Onyonka, hata hivyo, alisema kuwa Ford Kenya iko tayari kufanya mazungumzo na kiongozi yeyote kubuni muungano.

“Lakini Dkt Ruto hajawahi kuja kwetu akitaka tufanye muungano,” alisisitiza Bw Onyonka.

Mbunge huyo alisema kuwa matukio ya hivi karibuni ambapo Bw Wetang’ula ameonekana pamoja na Spika wa Seneti Kenneth Lusaka wakizunguka katika Kaunti ya Bungoma, si ushahidi kwamba Ford Kenya inafanya mazungumzo na Dkt Ruto.

Bw Lusaka ni mwandani wa Dkt Ruto.

“Spika Lusaka analenga kurejea katika Ford Kenya ndiposa amekuwa akiandamana na kiongozi wa chama katika hafla mbalimbali.

“Tuko tayari kuungana na chama chochote lakini wakati wa kufanya hivyo haujawadia. Kwa sasa muungano wetu ni OKA,” alieleza Bw Onyonka.

Naibu Rais anaendelea na mikakati ya kuwavutia Bw Wetang’ula na Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya, upande wake katika juhudi za kumega kiasi kikubwa cha kura za eneo la Magharibi mwaka ujao.

Gavana Oparanya amenukuliwa mara kadhaa akisema hana mpango wa kugura ODM.

“Ninaenda kufanya nini kwa Ruto. Katika ODM mimi ni naibu kiongozi. Kuna watu wanataka kunichafulia jina kwa kunihusisha na Naibu Rais, hawatafaulu,” alikariri Bw Oparanya.

Naye Spika Lusaka alisema ndoto ya jamii ya Waluhya kuungana itatimia tu endapo viongozi wataanza kuzungumza kwa sauti moja.

Kulingana na Spika huyo wa Seneti, mmoja wa viongozi wa jamii ya Waluhya atakuwa rais mwaka ujao watakapoungana.

“Jamii ya Waluhya ina idadi kubwa ya kura. Tukiungana na kisha tushirikiane na jamii nyingine tutaunda serikali ijayo,” alieleza Bw Lusaka.

Wakati huo huo, Kaimu Katibu Mkuu wa Ford Kenya, Bw Chris Wamalwa, amesema kuwa kamati maalumu ya OKA imeanza kutengeneza mwongozo utakaotumiwa kuhakikisha vyama vyote tanzu vinapata nyadhifa sawa katika serikali ijayo.

“Eneo la Magharibi limekuwa likitengwa serikalini kwa muda mrefu. Tutatumia idadi ya kura tulizonazo kuunga mkono mmoja wetu; Bw Mudavadi au Bw Wetang’ula, kuwania urais 2022,” akasema Bw Wamalwa, ambaye pia ni mbunge wa Kiminini.

You can share this post!

MKU yashirikiana na UN kuwajali wanaoishi na ulemavu

Cha kufanya ili uwe na uso laini na unaong’aa