• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Gavana Samboja aliyebwagwa uchaguzini ‘ashukuru’ wakazi kwa kura zao chache

Gavana Samboja aliyebwagwa uchaguzini ‘ashukuru’ wakazi kwa kura zao chache

NA LUCY MKANYIKA
Aliyekuwa Gavana wa Taita Taveta Granton Samboja alifanya ziara katika kijiji cha Mkamenyi, kaunti ndogo ya Voi  Alhamisi, Septemba 7, 2023 ambapo aliwashukuru wakazi kwa kumpa kura tano pekee katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.
Licha ya kupoteza azma ya kutetea kiti chake katika uchaguzi uliopita, Bw Samboja alisema anashukuru wakazi wa eneo hilo kwa kumpa kura, japo chache.
Katika kinyang’anyiro hicho, Samboja aliibuka wa pili kwa kura 23,703 huku Gavana Andrew Mwadime akiibuka mshindi na kura 49,901.
Akiongea katika eneo hilo, Bw Samboja alisema kuwa uongozi unatoka kwa Mungu na anashukuru kwa kura alizopata kutoka kwa wakazi hao.
“Nimerudi Mkamenyi kusema asante kwa kunipigia kura tano katika uchaguzi uliopita. Uongozi hutoka kwa Mungu. Ninasema asante,” alisema.
Gavana huyo wa zamani pia aliahidi kusaidia mwanafunzi mmoja wa eneo hilo ambaye anatazamiwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi mwezi huu.
Aliwataka wenyeji wa kaunti hiyo kuunga mkono viongozi badala ya kuwatoa katika uongozi kabla ya kutekeleza maendeleo.
Bw Samboja alisema kuwa tabia ya kuwatema viongozi baada ya kuhudumu kwa kipindi kimoja inalemaza maendeleo na kuifanya kaunti hiyo kubaki nyuma.
Katika mahojiano ya hivi majuzi katika kituo kimoja cha redio, Bw Samboja alisema hakuwa na uchungu wowote kwa kupoteza kura na kumtakia mrithi wake mema katika kuwatumikia wenyeji.
Alisema ataendelea kuwasaidia wenyeji wa Taita Taveta katika nyadhifa zingine na kuahidi kutoa usaidizi kila unapohitajika.
Alisema amekubali matokeo ya uchaguzi huo na kuwataka viongozi kufanya kazi kwa umoja kwa ajili ya kuleta maendeleo.
“Sina kinyongo naye (Andrew Mwadime) na pia kiongozi mwingine yeyote. Kipindi cha kampeni kilipita na sasa ni wakati wa kufanya kazi,” alisema.
Bw Samboja amekuwa akizuru maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo na kukutana na wakazi, akiwashukuru kwa kumuunga mkono katika uchaguzi uliopita.
Ziara za Samboja zinaonekana kama ishara ya kampeni za mapema za uchaguzi wa 2027.
Hata hivyo, Bw Samboja amepuuzilia mbali madai hayo na kuwataka wakosoaji wake kukoma kueneza uvumi na propaganda juu yake na kuzingatia masuala ya maendeleo.
“Nina haki ya kidemokrasia ya kuwania au kutowania nyadhifa yoyote katika uchaguzi ujao. Pia nina haki ya kwenda popote katika kaunti hii,” alisema.
Alimtaka Gavana Mwadime kuhakikisha kuwa anatimiza ahadi alizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni.
  • Tags

You can share this post!

Utafiti wabaini ARVs hutumika kunenepesha kuku, nguruwe

Kassait apendekeza Sheria ya Kulinda Data ya 2019 ifanyiwe...

T L