• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Haji arejeshea tena EACC faili za sakata ya Kemsa

Haji arejeshea tena EACC faili za sakata ya Kemsa

Na AMINA WAKO

KWA mara nyingine, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji ameirejeshea Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) faili zilizokuwa na ushahidi wa ubadhirifu wa fedha katika Mamlaka ya Kusambaza Vifaa vya Kimatibabu (KEMSA) unaokadiriwa kufikia Sh7.8 bilioni.

Hii ni baada ya afisi ya Bw Haji kupitia uchunguzi wake na kugundua kuwa kuna mapengo kadhaa kwenye ushahidi uliowasilishwa na EACC ambao hautoshi kuwashtaki washukiwa.

“Kuna masuala mengi ambayo yanahitaji kukamilishwa kuhusiana na uchunguzi wa ufisadi ndani ya Kemsa. Tunashirikiana na EACC kuhakikisha kuwa kesi itakayowasilishwa itakuwa thabiti na waliohusika waadhibiwe vilivyo. Huenda itachukua muda lakini mwishowe tutafanikiwa,” akasema Bw Haji.

EACC ilikuwa imewasilisha faili kwa ODPP mnamo Agosti 2020 ikiomba kuwashtaki watu sita kutokana na utoaji zabuni bila kufuata utaratibu unaohitajika pamoja na kutoa malipo bila kufuata sheria.

Hata hivyo, Bw Haji alisema kuwa baada ya kuchunguza faili zilizowasilishwa na EACC, wamegundua kuwa hakuna ushahidi na hivyo basi itabidi tume ya EACC izibe mianya iliyojitokeza kwenye ushahidi huo kwa kuanzisha uchunguzi mpya.

“Tumeangalia faili na kwa kweli hakuna ushahidi ambao utatuwezesha tuwapeleke washukiwa kortini. Ni jambo la kawaida kuwa tukiona mianya katika uchunguzi wowote basi tunarejesha faili kwa EACC ndipo uchunguzi zaidi uendelezwe,” akaongeza.

EACC ilifanya uchunguzi wake kwa siku 21 jinsi alivyoamrisha Rais Uhuru Kenyatta mara tu baada ya madai ya ufisadi kuibuka kwenye Kemsa mwaka 2020.

You can share this post!

Mkenya Jebet Tirop aweka rekodi mpya ya dunia mbio za...

Bayern Munich watua nafasi ya pili kwenye Bundesliga baada...