• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 8:50 AM
Bayern Munich watua nafasi ya pili kwenye Bundesliga baada ya kupepeta RB Leipzig

Bayern Munich watua nafasi ya pili kwenye Bundesliga baada ya kupepeta RB Leipzig

Na MASHIRIKA

BAYERN Munich walipaa hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mnamo Jumamosi usiku baada ya kupepeta RB Leipzig walioambulia nafasi ya pili mnamo 2020-21 kwa mabao 4-1 ugenini.

Kigogo Robert Lewandowski alifungulia Bayern ukurasa wa mabao kupitia penalti ya dakika ya 12. Bao hilo lilikuwa lake la sita kufikia sasa msimu huu wa 2021-22.

Chipukizi Jamal Musiala alipachika wavuni bao la pili la Bayern mwanzoni mwa kipindi cha pili kabla ya kuchangia goli la tatu lililofumwa wavuni na kiungo wa zamani wa Manchester City, Leroy Sane.

Ingawa Konrad Laimer alipania kurejesha wenyeji Leipzig mchezoni katika dakika ya 58, Bayern ya kocha Julian Nagelsmann walifungiwa bao la nne kupitia Eric Maxim Choupo-Moting sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Bayern ambao ni mabingwa watetezi wa Bundesliga sasa wanashikilia nafasi ya pili jedwalini kwa alama 10, mbili pekee nyuma ya viongozi VfL Wolfsburg waliokomoa SpVgg Greuther Furth 2-0 na kuendeleza rekodi ya kushinda mechi nne mfululizo za ufunguzi wa muhula huu.

Kwa upande wao, Leipzig sasa wamepoteza mechi tatu kati ya nne zilizopita chini ya kocha mpya Jesse Marsch aliyeaminiwa kuwa mrithi wa Nagelsmann mwishoni mwa msimu uliopita. Nagelsmann aliyoyomea Bayern kujaza pengo la kocha Hansi Flick aliyeajiriwa na timu ya taifa ya Ujerumani baada ya Joachim Loew kujiuzulu mwishoni mwa fainali za Euro 2020.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Haji arejeshea tena EACC faili za sakata ya Kemsa

Fidu aahidi makubwa kwa mashabiki wa Changamwe Ladies