• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Hamasisho lapunguza idadi ya wanaofariki wakijifungua Magarini

Hamasisho lapunguza idadi ya wanaofariki wakijifungua Magarini

NA ALEX KALAMA

IDADI ya wanawake wanaofariki wakati wa kujifungua katika eneo la Magarini imepungua kutokana na hamasisho linalotolewa kwa wajawazito wakihimizwa kujifungua hospitalini.

Kulingana na katibu wa muungano wa maafisa wa kujitolea wa afya ya nyanjani eneo la Magarini Micheal Katana, tangu kuanzishwa kwa hamasisho hilo, wanawake wengi wajawazito wamekuwa wakitembelea kliniki.

“Siku za nyuma kina mama wengi walikuwa wakipoteza maisha wakati wa kujifungua kutokana na hatua ya wao kujifungulia nyumbani, lakini sasa tangu wataalam wa uzazi walipojitolea kuihamasisha jamii kuhusu athari za kina mama kujifungulia nyumbani visa hivyo vimepungua kwa asilimia kubwa hususan hapa Magarini,” akasema Bw Katana.

Aidha, Katana amedokeza kuwa hatua hiyo imekuwa ikirahisisha huduma za matibabu kwa wanawake wajawazito katika hospitali mbalimbali za Kaunti ya Kilifi.

“Tangu hamasa ilifike mashinani zaidi ya asilimia 75 ya kina mama siku hizi wakiwa ni wajawazito hutembelea kliniki na hii inasaidia kuimarisha afya zao,” akasema Bw Katana.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa muungano huo Zawadi Mnyazi Randu amesisitiza haja ya serikali ya Kaunti ya Kilifi kuhakikisha kuwa hospitali zote za kaunti hiyo zina dawa za kutosha na vifaa vya huduma ya kwanza.

“Ombi letu kwa serikali ya kaunti ni kwamba tunataka ifanye kila iwezalo kuhakikisha kwamba zahanati zote zilizoko mashinani zinapata dawa na vifaa hitajika, wahudumu wa afya na pia chumba cha kina mama kujifungua,” alisema Bi Randu.

Aidha Bi Randu alisema iwapo serikali itaweza kuzingatia swala hilo na kulishughulikia ipasavyo basi hiyo itasaidia pakubwa kuboresha huduma ya afya kwa wananchi mashinani.

  • Tags

You can share this post!

Makundi ya kidini Kenya yasifu Rais Museveni kuharamisha...

Gachagua asimulia alivyozuru kanisa Kericho nusu ya waumini...

T L