• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
Matumaini teknolojia mpya ya kutibu ugonjwa wa selimundu ikifanyiwa majaribio

Matumaini teknolojia mpya ya kutibu ugonjwa wa selimundu ikifanyiwa majaribio

NA PAULINE ONGAJI

WAGONJWA wanaougua maradhi ya selimundu wana matarajio makubwa endapo teknolojia mpya ya matibabu inayofanyiwa majaribio na kamati ya ushauri katika Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini Amerika (FDA), itaidhinishwa.

Endapo yataidhinishwa, matibabu haya mapya kwa jina exa-cel, ambayo yamevumbuliwa na kampuni ya Amerika ya Vertex Pharmaceuticals na ile ya Uswisi ya CRISPR Therapeutics, yatakuwa ya kwanza kuidhinishwa kutumia teknolojia ya kubadilisha jenetiki, kwa jina CRISPR.

Teknolojia ya CRISPR, au clustered regularly interspaced short palindromic repeats, ambayo inatumika na watafiti, inahusisha kubadilisha DNA inayobeba mawasiliano ya kijenetiki na ambayo mwili hutumia kufanya kazi na kukua.

Kufikia sasa, matibabu ambayo yamekuwa yakitumika kutibu maradhi haya ni upasuaji wa kuhamisha uboho.

Nchini Kenya, upasuaji wa kwanza wa kuhamisha uboho ulifanywa mwezi Oktoba 2022, na japo kulingana na wataalamu hii ilitoa nafasi murwa kwa wagonjwa wa selimundu humu nchini kupokea matibabu, kulingana na FDA, utaratibu huu ni hatari na wakati mwingine huenda usiwe na matokeo au hata usababishe kifo cha mgonjwa.

Isitoshe, kulingana na shirika hili, ni wagonjwa chini ya asilimia 20 pekee ambao hupata mtoaji uboho anayeambatana nao.

Hata hivyo, tiba hii mpya ya exa-cel inaweza kutumia uboho wa mgonjwa husika.

Madaktari wanaweza ubadilisha kwa kutumia utaratibu wa CRISPR ili kurekebisha matatizo ya kijenetiki yanayosababisha selimundu, kisha uboho uliorekebishwa unarejeshwa katika mwili wa mgonjwa mara moja.

Kati ya wagonjwa 40 waliofanyiwa majaribio hayo, 39 hawakukumbwa na maumivu yanayotokana na maradhi ya selimundu (vaso-occlusive crisis), ambayo husababishwa na seli za damu zisizo na maumbo ya kawaida, ambazo huziba mzunguko wa damu na kusababisha maumivu.

Hii ndiyo sababu kuu inayowafanya wagonjwa wa selimundu kulazwa hospitalini.

Kabla ya majaribio haya, wagonjwa hawa walikuwa wanakumbwa na maumivu angaa mara nne kwa mwaka, suala lililowalazimu kulazwa hospitalini.

Mtafiti mkuu na daktari katika kituo cha kansa cha hospitali ya watoto ya Boston Dkt Daniel Bauer, aliliambia jopo hilo kwamba hatari ya kuwepo kwa athari za mabadiliko ya kijenetiki ambzao huenda zikatokea katika harakati za utaratibu huu na kusababisha kansa au matatizo mengine ni kidogo.

Bara la Afrika linawakilisha zaidi ya asilimia 66 ya watu milioni 120 wanaoishi na maradhi ya selimudu kote duniani, huku takriban watoto 1,000 wakizaliwa na maradhi haya hapa barani, kila siku.

Kulingana na utafiti, zaidi ya nusu ya watoto hawa wataaga dunia kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano, hasa kutokana na maambukizi au ukosefu wa seli nyekundu za damu za kutosha.

Barani Afrika, vifo 38,403 kutokana na maradhi ya selimundu, vilirekodiwa mwaka wa 2019, ongezeko la asilimia 26, kutoka mwala wa 2000, huku mzigo huu ukitokana na uwekezaji duni katika jitihada za kukabiliana na maradhi haya.

Kulingana na Dkt Gil Wolfe, ambaye ni mwanachama huru wa kamati hiyo, na profesa katika idara ya nyurolojia katika chuo kikuu cha matibabu na sayansi cha Buffalo Jacobs School of Medicine and Biomedical Sciences, matibabu haya ni mojawapo ya taratibu ambazo huenda zikasaidia wagonjwa wanaougua maradhi ya selimundu.

Hata hivyo, FDA haitarajiwi kufanya uamuzi wa kuidhinisha teknolojia hii hadi siku ya mwisho ambayo ni Desemba 8, 2023.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Rising Starlets waendelea kujifua dhidi ya Cameroon kuwinda...

Hasara mvua ikiendelea kuponda nchi

T L