• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Hisia mseto zaibuka baada ya Mwangaza kuokolewa na Seneti

Hisia mseto zaibuka baada ya Mwangaza kuokolewa na Seneti

GITONGA MARETE NA DAVID MUCHUI

VIONGOZI kutoka Kaunti ya Meru, wametoa wito wa umoja na utangamano licha ya mgawanyiko uliotokana na jaribio la kumng’atua uongozini Gavana Kawira Mwangaza, bunge la kaunti likionyesha kutoridhishwa na uamuzi wa Seneti.

Gavana huyo aliponea jaribio la kumng’atua madarakani kwa mara ya pili Jumatano usiku, baada ya maseneta kutupilia mbali mashtaka saba ambayo MCAs walikuwa wameyatumia kumtimua mnamo Oktoba 25.

Bi Mwangaza alishtakiwa kwa ubadhirifu wa fedha, mapendeleo, kuitaja barabara jina la mumewe Murega Baichu, kudharau agizo la mahakama na kuwatukana viongozi waliochaguliwa.

Mchakato wa kumtimua Bi Mwangaza ulichangia mzozo baina ya wabunge wa kaunti ya Meru na kuwahusisha wanasiasa wakuu, mtangulizi wake Kiraitu Murungi, waziri wa kilimo, Bw Mithika Linturi na naibu spika wa seneti Kathuri Murungi na wabunge wote tisa wa Meru.

Shangwe na Nderemo zilishuhudiwa Kaunti ya Meru baada ya gavana Mwangaza kuponea kung’atuliwa uongozini, huku wakazi wanaomuunga mkono wakisheherekea na kutaka viongozi kusuluhisha uhasama baina yao. Hata hivyo, wale ambao hawakuwa wakimuunga mkono walieleza kuwa Bi Mwangaza angetumwa nyumbani.

Wakazi kadhaa walitoa pia hisia zao mtandaoni kupongeza au kukashifu seneti kwa kumuokoa.

Kulingana na Bi Florah Igoki ambaye aliathirika na vita vya uchaguzi wa 2007 alipokuwa akiwania ubunge wa Imenti Kusini, alieleza kuwa uamuzi huo ulikuwa ushindi kwa uongozi wa wanawake.

Naye Bi Gakii Mbui alieleza kugadhabishwa kwake na hatua ya seneti akieleza kuwa shida za kaunti ya Meru zilikuwa nyingi.

“Hatua inayofuata ni kuvunja serikali ya kaunti kwa kuwa shida tunazopitia ni nyingi sana, hatujafurahia uamuzi wa seneti,” akasema Bi Mbui.

Mchakato huo katika bunge la seneti uliweka wazi uhasama wa kisiasa na mgawanyiko wa viongozi wa kaunti ya Meru, huku video zilizochezwa bungeni zikijawa na ubaguzi dhidi ya wanawake, wazungumzaji wa kambi za Azimio na Kenya Kwanza wakimkashifu Bi Mwangaza.

Licha ya hayo, Bi Mwangaza alikuwa tayari kuwasamehe wote waliohusika katika mzozo huo na kuomba msamaha kwa aliokuwa amewakosea.

Hapo jana, mahasibu wakuu wa Bi Mwangaza waliwataka wapinzani wake, kuzungumza na kumaliza uhasama.

“Tunataka kuwakaribisha viongozi wote, tufanye kazi pamoja kwa manufaa ya kaunti yetu. Kutaka kumtoa uongozini Bi Mwangaza kulikuwa njama ya viongozi kutok Nairobi. Nataka kuwaomba wabunge wetu na Bw Linturi kukubali kuwa Meru ina kiongozi,” akasema bw Gideon Kimanthi mshauri wa kibiashara wa Bi Mwangaza.

Katibu mkuu wa Njuri Ncheke Bw Washington Mbaya anayesimamia mipango na mwenzake Bw Josphat Murangiri, walieleza kuwa walikuwa wazi kwa upatanisho licha ya kuunga mkono kampeni ya kumbandua Bi Mwangaza uongozini.

“Hatumchukii gavana. Tunataka tu uongozi mzuri na iwapo atatukaribisha kwa mazungumzo tutaenda kwa kuwa hakuna chuki. Tunataka amani kwa ajili ya jamii ya Ameru,” akasema Bw Muthamia.



  • Tags

You can share this post!

Mahakama yakataa kuachilia Sh21 milioni za kulipia mahari

Nafikiria kumwambia baba simpendi mke wake wa pili

T L